Simba hasira zote kwa Biashara, Gwambina

Monday September 14 2020

 

By Mwandishi Wetu

BAADA ya kucheza mechi mbili ugenini sasa Simba wanajipanga kukusanya pointi sita katika mechi mbili watakazocheza uwanja wa nyumbani wa Benjamini Mkapa.

Mechi ya kwanza, Simba ilicheza Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya dhidi ya Ihefu FC ambapo mabingwa hao walishinda bao 2-1.

Mechi ya pili, Simba ilicheza na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro ambapo timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 na hivyo kurejea jijini Dar es Salaam ikiwa imekusanya pointi nne.

Hivi sasa, Simba inajiandaa kuikaribisha Biashara United ya mjini Musoma ambapo watacheza Septemba 20, 2020 na baadaye kuikaribisha Gwambina FC ya wilayani Misungwi, Mwanza.

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara amesema kwamba wachezaji wao wamepewa mapumziko ya siku moja ambapo kesho Jumanne Septemba 15, 2020 wataingia kambini ambapo kocha wao Sven atatoa programu ya mazoezi.

"Mechi za ugenini ni ngumu, tumepata pointi nne kati ya sita, ni kama asilimia 75 za pointi, hatuko katika hali mbaya kama baadhi wanavyoelezea.

"Kikubwa sasa ni kujipanga na michezo ijayo ambayo tutakuwa nyumbani dhidi ya Biashara United na Gwambina FC, tuna faida ya kupata matokeo nyumbani kwasababu uwanja ni wetu, uwanja tumeuzoea na wachezaji wanauelewa vizuri ingawa mechi zote ni ngumu," amesema Manara.

Baada ya mechi hizo mbili, katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ambapo timu kila timu imecheza mechi mbili, Simba ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo wanasimama nafasi ya tano huku wakiongozwa na KMC wenye pointi sita sawa na Azam FC, Dodoma Jiji na Biashara United tofauti yao ni mabao ya kufunga na kufungwa.

Advertisement