Simba buana yampeleka Kiulaini Masoud Jangwani

Masoud Djuma

Muktasari:

Simba imemsitishia mkataba Kocha wake Msaidizi, Masoud Djuma na kutoa nafasi kubwa ya Kocha huyo kutua kokote, lakini Yanga inasaka kocha wa kuchukua nafasi ya Shadrack Nsajigwa aliyetimka klabuni na kwa namna hali ya mambo ilivyo, Mrundi huy anaweza kuwa mtu sahihi kutua Jangwani kwa sababu ya rekodi zake kumbeba.

HAKUNA ubishi tena, ndoa ya Kocha Mrundi, Masoud Djuma na Simba imefikia mwishoni, hata kama pande zote zimekuwa zikichenga kuanika ukweli. Kikao cha muda mrefu kilichofanyika juzi jijini Dar es Salaam kinathibitisha ndoa imevunjika rasmi.

Minong’ono ya Kocha Masoud kutemwa Msimbazi ilianza siku nyingi, japo mabosi wa Simba walikuwa wakificha na kikubwa ni kudaiwa kutoiva na Kocha Mkuu, Patrick Aussems ambaye amekuwa akimlalamikia kwa mabosi eti hana nidhamu.

Mbali na tuhuma hizo, lakini Masoud inadaiwa hata baadhi ya viongozi kutokana na kukubalika kwake kwa mashabiki na kuigawa Simba.

Baadhi ni kutojumuishwa katika msafara wa timu hiyo pindi ilipoenda kucheza mechi tatu mfululizo za ugenini katika Ligi Kuu dhidi ya timu za Ndanda, Mbao na Mwadui huku akiachiwa wachezaji ambao hawakusafiri na wale wa kikosi cha vijana awanoe ilikuwa ni moja ya dalili za wazi hatakiwi Msimbazi.

Hata baada ya kurejea jijini na kisha kucheza na Yanga, Masoud japo alikuwa sehemu ya timu, katika mazoezi ya Simba majukumu ya kumsaidia Aussems kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakifanywa na kocha wa viungo Adel Zrane, Mrundi akiwa kama mtazamaji tu.

Ndani ya nafsi yake, Masoud anajua na kufahamu mwenyewe wapi ataelekea baada ya kutoka Simba lakini uamuzi wa Yanga kumchukua kocha huyo baada ya kuachana na watani wao unaweza kuwa na manufaa makubwa kwa pande zote mbili.

Kwa nini kila upande utanufaika ikiwa Masoud atatua Jangwani baada ya kuachana na Simba? Mwanaspoti linakudadavulia kwa uchache.

KUIATHIRI SIMBA KISAIKOLOJIA

Hakuna asiyefahamu utamaduni wa klabu hizi mbili kongwe nchini kutopenda kuona au kufurahia mafanikio ya upande mwingine ambao umekuwa ukidumu vizazi hadi vizazi.

Kitendo cha Yanga kumchukua Masoud, kitawaweka kwenye nafasi nzuri ya kupunguza hali ya kujiamini kwa Simba kwani itahisi na kuamini kocha huyo atawapa watani wao siri ya mbinu na mikakati yao na hivyo kuwapa nguvu zaidi katika vita ya Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Simba huenda wakataka kutumia nguvu kubwa zaidi kwa lengo la kuonyesha inaweza kufanikiwa bila Masoud, jambo linaloweza kuwaweka kwenye presha itakayonufaisha wapinzani wao.

Iliwahi kutokea kwa mshambuliaji Amissi Tambwe alipotua Yanga ambapo alitumia udhaifu wa Simba kumpania, kuwafunga katika mechi tatu mfululizo na kuingia kwenye rekodi akilingana na Shiza Kichuya na Madaraka Selemani wote wa Simba.

KUTHIBITISHA UWEZO

Yanga chini ya Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera ambaye pia ni kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imekuwa ikiyumba, pale Mkongo huyo anapokwenda kutekeleza majukumu yake ya kitaifa kwao.

Timu hubaki na Msaidizi wake, Noel Mwandila, ambaye rekosi zinaonyesha hajawa na maajabu akikiongoza kikosi hicho katika mechi mbalimbali tangu alipotimka Mzambia George Lwandamina na hata anapompokea kijiti kwa muda Zahera.

Hivyo kama Masoud atatua Jangwani na akienda kwenye majukumu ya kimataifa, ni wazi Yanga itakuwa mikono salama kwani Mrundi huyo rekodi zake Msimbazi zinambeba.

Ikumbuke Noel alikuja nchini kama kocha wa viungo, hivyo ni wazi kwa ukubwa wa daraja la leseni ya ukocha na historia aliyonayo Masoud, iwapo akienda Yanga yeye ndio atakuwa msaidizi mkuu wa Zahera.

Masoud atakuwa na nafasi kubwa ya kuthibitisha uwezo wake kwani ndiye atakuwa anasimamia timu mara kwa mara tofauti na sasa analazimika kusikiliza tu maagizo ya benchi la ufundi.

KUNASA NYOTA WA SIMBA

Moja ya jambo lililomjengea umaarufu mkubwa Masoud ndani ya Simba ni jinsi alivyofanikiwa kutoa nafasi kwa kila mchezaji kuonyesha kipaji chake pindi alipopewa jukumu la kuinoa kwa muda baada ya kutimuliwa kwa Joseph Omog.

Hata hivyo, baada ya Masoud kurejea kwenye majukumu ya ukocha msaidizi chini ya Pierre Lechantre na baadaye Aussems, baadhi ya wachezaji ambao walipata nafasi ya kucheza chini yake wamejikuta wakisotea benchi na wengine kutazama mechi wakiwa jukwaani.

Hata hivyo, pamoja na wachezaji hao kutopata nafasi ya kucheza, wengi wana viwango vya juu na wanaweza kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga.

Kumchukua Masoud inaweza kuwa karata nzuri kwa Yanga kuwanasa kirahisi wachezaji hao, ikitumia ushawishi na ukaribu ambao anao kwa nyota hao wanaosugua benchi.

KULETA MPASUKO MSIMBAZI

Masoud amefanikiwa kuteka hisia za mashabiki, wapenzi na kundi kubwa la wanachama wa Simba ambao wengi wao wanaamini na kuhisi kuwa anastahili kuwa kocha wao mkuu na yote yanayomtokea kwa sasa ni chuki binafsi za kocha mkuu na baadhi ya viongozi.

Ikiwa Yanga itamchukua Masoud, kundi kubwa la mashabiki, wapenzi na wanachama wa klabu wa Simba hawatofurahishwa na hali hiyo na huenda ikasababisha maelewano na ushirikiano duni baina yao na uongozi, jambo linaloweza kuinufaisha Yanga, kwa vile kuvuja kwa pakacha...!

LUGHA INAMBEBA

Kocha Mwinyi Zahera anazungumza lugha mbili kwa ufasaha ambazo ni Kifaransa na Kilingala na amekuwa akizungumza lugha ya Kiswahili kwa tabu mno jambo ambalo wakati mwingine linaweza kupelekea wachezaji wasishike na kuelewa kwa usahihi kile anacho waelekeza.

Uwepo wa Masoud utamfanya Zahera aweze kuwasiliana vizuri na wachezaji wake kwani Raia huyo wa Burundi anaweza kuzungumza kwa ufasaha lugha ya Kifaransa na Kiswahili ambayo ndio inatumiwa na idadi kubwa ya wachezaji wa Yanga.

HAMASA

Moja ya sifa za Masoud ni uwezo wake wa kuhamasisha na kupandisha ari na molali ya wachezaji pamoja na mashabiki pindi wanapokuwa uwanjani jambo linaloweza kuifanya timu kuhamasika na kupambana kusaka matokeo.

Yanga itakuwa imepiga bao ikimchukua Djuma kwani atawatimizia vyema jukumu hilo ambalo mara kwa mara limekuwa likifanywa na kocha wa makipa, Juma Pondamali ‘Mensah’.