Simba Mwanza wapata mabosi wapya

Thursday June 27 2019

 

By Saddam Sadick

MSIMU uliopita timu za Mbao na Kagera Sugar ziliitesa Simba, sasa unaambiwa uongozi mpya wa Simba uliochaguliwa mkoani hapa umeahidi msimu ujao kufa na timu hizo.

Katika uchaguzi uliofanyika juzi jijini hapa uliwachagua, Philemon Tano kuwa Mwenyekiti wa Simba Mkoa wa Mwanza, Ishuu Ashrafu (Makamu), Filbert Kabago (Katibu Mkuu) na Mohamed Hamis ambaye ni Mweka Hazina.

Wajumbe ni Salya Ludanha, Nemes Damas na Fatuma Shemweta ambao wataiongoza Simba ngazi ya Mkoa wa Mwanza kwa kipindi cha miaka minne.

Wakizungumza baada ya uchaguzi huo, viongozi hao waliahidi kuhakikisha msimu ujao Simba inapata ushindi kwa mechi zote za Kanda ya Ziwa huku wakisisitiza umoja.

Kabago alisema msimu uliopita Simba ilipoteza mechi tatu kwa timu za Kanda ya Ziwa, hivyo msimu ujao hawatakubali tena Chama lao kufungwa. Simba walifungwa na Mbao bao 1-0, walipoteza dhidi ya Kagera Sugar bao 2-1 ambao waliwafunga na Taifa bao 1-0.

“Lazima tuungane kwa pamoja na sisi mliotuchagua tutahakikisha hatuwaangushi, tutapambania timu yetu kushinda mechi zote za Kanda ya Ziwa ikiwa ni nyumbani na ugenini,” alisema Kabago.

Advertisement

Naye Ludanha aliyepita nafasi ya Ujumbe, alisema ili kufikia malengo lazima mashabiki na wanachama wawe na umoja na kwamba furaha yao ni kuona Simba ikifanya vizuri kitaifa na kimataifa.

“Binafsi niwaahidi umoja na mshikamano kwa kipindi chote cha miaka minne, tunachotaka ni kuona Simba inafanya vizuri katika mashindano yake, tunaomba ushirikiano tufikie malengo,” alisema Ludanha.

Advertisement