Simba Mwanza kuwabana wauza jezi feki

Makamu Mwenyekiti wa Simba Mkoa wa Mwanza, Ashuu Ashraf (wa pili kutoka kushoto) akizungumza wakati wa uzinduzi wa Ofisi ya Klabu hiyo Mkoa wa Mwanza.

Muktasari:

Ofisi hiyo ambayo imezinduliwa leo Julai 20 itakuwa ikiuza vifaa vya michezo vya Klabu hiyo kwa bei elekezi,ambapo uzinduzi huo umeshirikisha viongozi wa Mkoa na matawi ya Simba Mkoa wa Mwanza.

VIONGOZI wa Simba Mkoa wa Mwanza wamesema watakuwa makini kuwashughulikia wafanyabiashara na wale ambao watabainika kuuza jezi feki msimu ujao kwa maslahi ya klabu yao.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Ofisi ya Simba Mkoa, Katibu Mkuu wa timu hilo, Pilibert  Kabago amesema uongozi utachukuwa hatua hiyo kwa wale watakaouza jezi feki na kuwarudisha nyuma kibiashara.
“Hiyo ni kujipatia fedha kinyume na utaratibu, sisi viongozi tuliopo mkoani lazima tusimamie maslahi ya Klabu ili kusonga mbele, timu inahitaji vitu vingi, hivyo hatutafumbia macho wale wanaotuhujumu,” amesema Kabago.
Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, Ishuu Ashraf amesema ili Simba iendelee kuwa juu lazima mashabiki na wanachama kuungana kwa pamoja kuendelea kuwa mbele.
“Leo tunazindua Ofisi hii ya Mkoa kama utekelezaji wa ahadi yetu tangu kuingia madarakani na niseme tu si kwa nguvu ya mtu yeyote bali ni umoja na mshikamano wetu”amesema Ashraf.
Naye shabiki wa kulia wa Wekundu hao, Aleem Alibhai amesema Wanasimba lazima wafahamu kuwa mpira una matokeo matatu, ikiwa ni ushindi, sare na kupoteza.
“Ikiwa tutashikamana Simba itaendelea kutwaa makombe, lakini niwasihi kwamba lazima tutambue mpira una matokeo matatu hivyo tuendelee kuisapoti timu ili ipate ushindi tu” amesema Alibhai.