Simba Moro wapiga dua kwa saa mbili kumuombea MO

Muktasari:

Wanachama wa Simba wamekuwa wakifanya kisomo na kuomba dua tangu jana ili mfadhili wao MO Dewji apatikane akiwa hai

Morogoro. Wanachama wa matawi manne ya klabu ya Simba SC Manispaa ya Morogoro wametumia muda wa saa mbili kusoma dua kwa ajili ya kumuomba Mwenyezi Mungu kumnusuru na adha yoyote dhidi ya watu waliomteka, Mfanyabiashara Mohamed Dewji (Mo).

Akizungumza baada ya kumalizika kwa kisomo ofisi ya tawi ya Simba tawi la Shujaa Soko la Mjipya mkoani hapa, Mjumbe wa kamati tendaji ya matawi ya Simba SC mkoa wa Morogoro, Hashimu Mdoe alisema lengo la kusoma dua hiyo ni kumuomba Mwenyezi Mungu kumnusuru, Mo Dewji na watekaji ili wamwachie akiwa salama na mwenye afya njema.

Mdoe alisema wanachama na wapenzi wa klabu ya Simba SC wameshtushwa na tukio hilo na kuwa linatia doa kwa nchini kutokana na Mohamed Dewji si kujishughulisha na michezo pekee bali amekuwa ni miongoni mwa wawekezaji wazawa.

“Tukio la kutekwa kwa Dewji sio kwamba limeathiri Simba SC pekee bali na watanzania kiujumla na limeba taswira nyingi kutokana na uwekezaji wake nchini kama mwekezaji mzawa.”alisema Mdoe.

Mdoe alisema kuwa yeye na wanachama na wapenda michezo nchini wana imani kubwa kutokana na juhudi zilizoonyeshwa na vyombo vya dola tangu siku ya kwanza ya kumtafuta kuhakikisha anapatikana.

Mwenyekiti wa Simba tawi la Shujaa Mjipya, Saidi Mkwinda alisema wamelazimika kama uongozi mkoani Morogoro kuunga juhudi za uongozi wa klabu ya Simba SC makao makuu wa kuongeza nguvu katika kuomba dua ya heri ili mfadhili Mo anasuke kwenye mikono ya watekaji akiwa salama.

Mkwinda aliyataja matawi yaliyotoa wawakilishi katika kusoma dua hiyo kuwa ni, Kilakala, Kinglwila Kichangani na Shujaa yenyewe iliyobeba tawi kuu la Simba sc mkoa wa Morogoro.

Katibu wa tawi la Simba SC Kilakala, Sharifa Saidi alisema kuwa kwa sasa wanachama, wapenzi na wadau wa soka Manispaa ya Morogoro wapunguze presha na kuwaomba kuongeza juhudi za kufanya maombi ili mwenyezi mungu awalekeze akili waliomteka Mohamed Dewji na kumwachia. 

“Ninachowaomba wanachama, mashabiki wa klabu ya Simba SC na wadau wa soka nchini kuzidisha maombi ili watekaji wawe na huruma kwa Dewji kumwachia huru akiwa salama na bila masharti,”alisema Sharifa.