Simba, Yanga wakwaa kisiki kwa beki Mnyarwanda

Tuesday November 6 2018

 

By MWANAHIBA RICHARD

KLABU za Simba na Yanga ziliingia kwenye vita ya kuwania saini ya beki Mnyarwanda Abdoul Rwatubyaye lakini masharti yaliyotolewa na mchezaji huyo ni magumu ambayo klabu hizo ziliamua kunyoosha mikono juu.
Beki huyo anayeichezea timu ya Rayon Sport ya Rwanda kwa sasa anatarajia kujiunga na timu ya Anderlecht FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji hapo Januari mwakani.
Meneja wa mchezaji huyo, Patrick Gakumba 'Super Meneja' aliliambia Mwanaspoti malengo ya mchezaji wake ni kucheza soka la kimataifa ila alikuwa tayari kutua nchini endapo moja ya klabu hizo zingekubali kumpa pesa ya usajili Dola 80,000 na mkataba wake uwe huru.
Mbali na masharti hayo mawili, pia sharti lingine ni kuilipa klabu yake asilimia 20 kama atapata timu nyingine nje ya Afrika.
"Wote wameshindwa hayo masharti, hivyo anasubiri kwenda Ubelgiji, Yanga wao hata pesa ya usajili wanataka kupunguziwa ila kwa Simba wamekataa sharti la kumpa mkataba usiombana maana hata wao wanashiriki michuano ya kimataifa," alisema Kagumba.
Tayari kocha wa Yanga, Zahera Mwinyi ameweka wazi mipango yake ya usajili na ametaja usajili wa wachezaji watatu akiwemo Mgabon Guylain Kisombe kutoka timu ya Mounana Gabon ambaye anacheza nafasi mbili beki na kiungo, pia atasajili straika mmoja na winga mmoja.
Upande wa Simba, Kocha Patrick Aussems naye ameweka wazi anahitaji straika mwenye uwezo mkubwa kufunga na kutengenza nafasi za mabao na baada ya msimu kumalizika ndiyo atasajili wachezaji wengine ambao atakuwa amewapa majina mabosi wake.

xxxxx

Advertisement