Sikia kilichompeleka De Ligt Juve

Muktasari:

De Ligt alisema magwiji wengi aliokuwa akiwapenda tangu utotoni katika nafasi yake anayocheza walikuwa wanacheza soka Italia.

TURIN, Italia.BEKI Matthijs de Ligt ameanza maisha mapya huko Italia na amefunguka kilichomvutia kumwaga wino Juventus huku akikana ushawishi wa Cristiano Ronaldo ndiyo uliompeleka Turin.
Klabu kadhaa kubwa za Ulaya zikiwamo Barcelona na Manchester United ziliripotiwa kumfukuzia beki hiyo mwenye mwili jumba lakini akaamua kutua Juventus ambao wamemwaga Euro 75 milioni ili kuinasa saini yake.
Katika mahojiano na Ajax TV, De Ligt alifunguka: "Ulikuwa ni uamuzi mgumu. Nilikuwa na machaguo mengi na nilipaswa kuchagua lililo bora zaidi.”
De Ligt alisema magwiji wengi aliokuwa akiwapenda tangu utotoni katika nafasi yake anayocheza walikuwa wanacheza soka Italia.
"Napenda mabeki wa Italia wanavyokaba na hilo lilichangia mimi kufanya uamuzi huu.
"Magwiji wangu wengi walicheza soka Italia: Baresi, Maldini, Nesta, Scirea... naweza kuendelea, ni wengi," alisema.
“Baada ya mechi ya fainali ya Nations League tayari nilikuwa nina uhakika kwamba nataka kuja Juventus, lakini bado ni heshima kubwa kwa Cristiano kuniomba nije huku, lakini haikubadili chochote,” alisema katika mkutano wake wa kwanza akiwa mchezaji wa Juve.