Sifa hizi uwe nazo, ama sivyo Simba utaisikia tu

Friday September 14 2018

 

By MWANAHIBA RICHARD

MWANAHIBA RICHARD

JANA Alhamisi tuliona sifa za mikutano ya Simba katika mfululizo wa makala za Katiba Mpya ya klabu hiyo.

Katiba hiyo imeainisha aina ya mikutano ya Simba na namna inavyoendeshwa katika kufanya uamuzi wake. Leo Ijumaa tutaangalia zaidi sifa za wagombea wanaojitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi, ambapo kama huna vigezo na sifa hizi basi nenda katafute kazi nyingine, vinginevyo ataishia kusikia wengine tu wakiitwa viongozi wa Simba. Kivipi? Endelea nayo...!

IBARA YA 27:

Sifa za Wagombea

1. Kutakuwa na wajumbe wanane watakaoiwakilisha Simba Sports Club katika Bodi ya Wakurugenzi; sita (6) wa kuchaguliwa na wawili (2) wa kuteuliwa ambao kati yao;

(a). Mjumbe mmoja atachaguliwa kama Mwenyekiti, na ni lazima awe na taaluma kiwango cha chini elimu ya angalau shahada ya kwanza au sifa inayolingana na hapo kutoka chuo kikuu kinachotambulika na Taasisi ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

(b). Mjumbe mmoja (1) lazima awe na taaluma, kiwango cha chini cha elimu ya angalau shahada ya kwanza au sifa inayolingana na hapo kutoka chuo kikuu kinachotambulika na TCU.

(c). Wajumbe wengine wanne wa kuchaguliwa waliobaki wanatakiwa kuwa na elimu isiyopungua kidato cha nne na angalau mjumbe mmoja wapo kati yao awe mwanamke.

(d). Wajumbe wawili watateuliwa na mwenyekiti kutoka miongoni mwa wanachama ambao, ni lazima wawe na taaluma ya angalau kidato cha nne.

2. Mtu yeyote anayegombea nafasi yeyote ya Simba Sports Club hana budi kutimiza masharti yafuatayo;

i. Awe na sifa zinazotakiwa kwa nafasi husika na amelipa ada ya uanachama kikamilifu tangu alipoanza uanachama.

ii. Awe na kiwango cha chini cha elimu kama ilivyoanishwa katika ibara ya 27 (1) (a) (b) na (c.

iii. Kiongozi wa kuchaguliwa atakaa madarakani kwa vipindi viwili tu vya kupiga kura kwa nafasi ya uongozi. Endapo atataka kurejea madarakani baada ya kutumikia vipindi viwili mfululizo, itabidi asubiri kwanza kupita kwa walau uchagizi mkuu mmoja wa kikatiba.

iv. Asiwe aliyewahi kutiwa hatiani kwa kosa la jinai kwa kuhukumiwa kifungo.

v. Awe na umri angalau miaka 25

vi. Awe ametimiza angalau miaka mitatu ya uanachama.

vii. Asiwe mwamuzi wa mchezo wa mpira wa miguu anayefanya shughuli za uamuzi kwa kipindi hicho.

viii. Mwanachama mwenye umri wa miaka 65 na kuendelea hataruhusiwa kugombea.

IBARA YA 28:

Marekebisho ya Katiba na Kanuni

1. Mkutano Mkuu una jukumu la kurekebisha Katiba na Kanuni Kuu za Mkutano Mkuu.

2. Pendekezo lolote la marekebesho ya Katiba halina budi kuwasilishwa na mwanachama/ wanachama kwa Sekretarieti. Pendekezo linalowasilishwa na mwanachama ni halali, alimradi limeungwa mkono kwa maandishi na angalau wanachama wengine mia moja (100) na kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Wanachama na Mashabiki siku 21 kabla ya Mkutano Mkuu.

3. Kwa kura inayohusu marekebisho ya Katiba kuwa halali, lazima wanachama halali wanaostahili kupiga Kura wawe zaidi ya nusu (50% +1).

4. Pendekezo la marekebisho ya Katiba litapitishwa endapo 2/3 ya wanachama wenye haki ya kupiga kura watakaopiga kura na watakubaliana nalo.

5. Pendekezo la marekebisho ya kanuni zinazohusu matumizi ya Katiba na Kanuni za Mkutano Mkuu, lazima ziwasilishwe kwa maandishi kwa Sekretarieti siku 21 kabla ya Mkutano.

6. Pendekezo la marekebisho ya matumizi ya Katiba na Kanuni Kuu za Mkutano Mkuu, litapitishwa tu iwapo zaidi ya nusu ( 50%+1) ya wanachama waliohudhuria na wanaostahili kupiga kura watakubaliana nalo.

Unajua Simba itakuwa na mabadiliko makubwa ya kiuendeshaji na majukumu ya wajumbe wa Bodi na adhabu kwa watakaokwenda kinyume? Fuatilia leo kesho Jumamosi.

Advertisement