Shungu: Tuisila na Mukoko, kocha tu ajue kuwatumia

Muktasari:
Yanga imekamilisha usajili wa wachezaji wawili kiungo wa kati Mukoko Tonombe na winga Tuisila Kisinda wakitokea klabu ya AS Vitta baada ya kumtuma mmoja wa viongozi wao.
KOCHA Msaidizi wa AS Vita, Raoul Shungu amesema Yanga imefanya usajili mzuri kupata wachezaji wawili bora kutoka kikosi chao pia amepongeza hatua za usajili huo zilizofanywa na uongozi wa klabu hiyo.
Shungu amesema Yanga kuwapata kiungo wa kati Mukoko Tonombe na winga Tuisila Kisinda ni moja kati ya usajili bora katika kikosi chao.
Shungu amewalezea wachezaji hao kwamba ni silaha nzuri kwa Yanga kutokana na uzoefu wao pamoja na ubora wao ambavyo vitaisaidia timu hiyo.
"Hapa Vitta makocha tuliambiwa kwamba Tuisila na Mukoko wataondoka, ni wachezaji ambao walikuwa bora lakini mpira ni biashara," amesema Shungu.
"Nafurahi kuona wote wanakwenda timu moja na ni timu yangu naipenda hapo Tanzania, wataisadia sana Yanga hawa wachezaji kocha ajue tu jinsi ya kuwatumia."
Shungu amesema hatua ya Yanga kumtuma bosi wao jijini Kinshasa nchini DR Congo kwenda kukamilisha usajili huo ni ukomavu wa uongozi wamefanya.
Kocha huyo wa zamani wa Yanga, amesema zamani Yanga haikuwa inafanya hivyo na kusababisha malumbano wakati wa usajili lakini sasa wameonekana kubadilika.
"Sijakutana na huyu kiongozi wao ila nina namba yake nitamtafuta, wamefanya ustaarabu mkubwa unahitajika kufanyika zamani mambo hatakuwa hivi.
"Hapa hata viongozi wa Vitta nao wamefurahi kuona wanaheshimika kwa kufuatwa na kumalizana vizuri." amesema Shungu