Shoo ya Gwambina, Pamba sasa Kirumba

Saturday June 27 2020
Gwambina pic

NI kufa au kupona. Ndio lazima kieleweke leo wakati Pamba na Gwambina zitakaposhuka uwanjani kuwania pointi tatu katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza, ambao utaamua hatma ya Gwambina kupanda Ligi Kuu msimu ujao, huku goma likipelekwa CCM Kirumba, jijini hapa.
Awali mtanange huo ulipangwa kupigwa Uwanja wa Nyamagana, lakini kwa sasa limehamishiwa Kirumba na Gwambina baada ya kushindwa kutangaza kupanda Ligi Kuu katika mchezo uliopita dhidi ya Transit Camp kwa kutoka sare ya 1-1, leo ikishinda tu freshi inazifuata Simba na Yanga.
Kwa sasa Gwambina ina pointi 41 katika nafasi ya kwanza, inahitaji ushindi wa aina yoyote ili kupanda Ligi Kuu huku Pamba ipo nafasi ya nane kwa alama 25 kwenye kundi B.
Hata hivyo, Pamba nayo haitakuwa na kazi rahisi kwani ikipoteza mechi hiyo inaweza kujikuta kwenye hali mbaya sana ya kushuka daraja, hivyo huenda leo ikashuhudiwa mechi kali na tamu.
Beki wa kati wa Gwambina FC, Revocatus Mgunga alisema akili zao zinawaza mechi hiyo muhimu na kwamba wataingia uwanjani kucheza kufa na kupona ili kutangaza kupanda Ligi Kuu.
“Kwa ujumla ni mchezo muhimu sana kwetu tunahitaji ushindi ili kutangaza kupanda Ligi Kuu, wachezaji tumejipanga vizuri na tunasubiri muda ufike twende kuandika historia” alisema Nyota huyo wa zamani wa Mwadui FC.
Katika mfululizo wa ligi hiyo ambayo jana kwenye Uwanja wa Uhuru, Pan African ikivaana na Boma FC,  leo kuna ngoma nyingine nane zinapigwa, ikiwamo za Kundi B kwa Green Warriors na Transit Camp zitaumana Dar es Salaam, huku Geita kunaa dabi ya Gipco dhidi ya Geita Gold.
Chama la Wana 'Stand United' ikiwakaribisha Machalii wa Arachuga 'AFC', na Rhino Rangers atacheza na Mashujaa FC Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.
Kundi A, Majimaji atacheza na Dodoma, Ihefu FC ikivaana na Afrcan Lyon, Mbeya Kwanza na Friends Rangers huku Iringa United ikiikaribisha Cosmopolitan, huku kesho Jumapili kutakuwa na mchezo mmoja kati ya Mlale iliyokumbana na rungu la kucheza bila mashabiki ikiikaribisha Njombe Mji kwenye Uwanja wa Majimaji.

Advertisement