Shoo kali ya wanaume

Friday November 8 2019

 

By Thobias Sebastian

TANZANIA Prisons ndio timu pekee ambayo haijapoteza mchezo licha ya jana Alhamisi kukutana na mabingwa watetezi na vinara wa ligi Simba.

Katika mchezo huo ambao ulipigwa Uwanja wa Uhuru, ulimalizika kwa suluhu pengine tofauti na ilivyotarajiwa na wapenzi wengi wa soka haswa kutokana na makali ambayo inayo Simba msimu huu.

Mwanaspoti ambalo lilikuwa uwanjani hapo lilifanya tathmini ya kila mchezaji wa Simba na Prisons ambao walicheza jana na kukupa alama ambazo alipata na kila mmoja akipata chini ya kumi.

AISHI MANULA - 4

Hakuonekana kupata mashambulizi mengi ila yale machache ndani ya dakika 90 alionekana kufanya makosa, kama kucheza mipira ya krosi na baadhi ya mastuti alishindwa kuyadhibiti kwa ufasaha.

SHOMARY KAPOMBE - 5

Advertisement

Aliweza kucheza vizuri kwa kutimiza majukumu yake ya kukaba washambuliji wa Prisons lakini katika kushambulia ilikuwa alikuwa hapewi mipira mingi.

‘TSHABALALA’ - 4

Beki wa kushoto wa Simba, alikuwa anafanya majukumu ya kushambulia na kufika lango la timu pinzani mara kwa mara lakini katika kukaba alikuwa akifanya makosa mengi.

ERASTO NYONI - 6

Beki wa kati alikuwa akicheza kwa maelewano na Pascal Wawa na muda mwingi waliweza kuwakaba washambuliaji wa Prisons, Samson Mbangula na Ismail Aziz kutokuleta madhara.

PASCAL WAWA - 5

Kuna muda alionekana kufanya makosa ya kiulinzi ambayo Nyoni alikuwa akiyaziba na mpaka mpira unamalizika hakuwa katika kiwango kizuri.

JONAS MKUDE - 3

Alikuwa akicheza katika nafasi ya kiungo mkabaji lakini muda mwingi alionekana kufanya makosa ya kiulinzi, kupoteza mipira na alizidiwa kumfanya kucheza katika kiwango cha kawaida kuliko ambavyo amezoeleka. Inaonekana dhihiri kwamba Mkude bado hajarudi katika kiwango chake baada ya kukosekana kwenye mechi za hivi karibuni za timu yake.

IBRAHIM AJIBU - 5

Alikuwa akipoteza mipira alishindwa kuanzisha mashambulizi na kupiga pasi za mwisho sahihi kama ambavyo alikuwa akifanya katika mechi za nyuma na mpaka anatoka na kuingia Deo Kanda alikuwa amecheza katika kiwango cha chini.

SHARAFELDIN SHIBOUB - 4

Alikuwa akicheza katika nafasi ya kiungo mshambuliaji, kipindi cha kwanza alikuwa akipoteza mipira na kuporwa na viungo wa Prisons na hakupiga pasi za mwisho kwa Kagere na alishindwa kufunga.

MEDDIE KAGERE -5

Mabeki wa kati wa Prisons, Vedastus Mwihambi na Nurdin Chona waliingia na mpango wa kumzuia muda wote jambo ambalo lilimfanya Kagere kushindwa kuonesha makali yake licha ya kuonekana kuhangaika huku na kule uwanjani bila ya mafanikio.

CLETOUS CHAMA - 4

Alikuwa akicheza nyuma ya mshambuliaji lakini muda mwingi alionekana kushuka chini katika eneo la kiungo kufuata mipira ambayo hata alipofanikiwa kuichukua alishindwa kusababisha madhara. Chama alitoka na kuingia Hassan Dilunga.

FRANCIS KAHATA - 5

Beki wa kushoto wa Prisons Laurian Mpalile alifanikiwa kumzuia Kahata ambaye muda mwingi alikuwa akipiga pasi fupi za nyuma na siyo zile za mbele ambazo zingewapa madhara timu pinzani. Kahata alikuwa akicheza kama vile anaogopa kugusana na wenzake kwani alichezewa faulo nyingi.

Tanzania Prison

JEREMIA KISUBI - 4

Kipa wa Prisons hakuwa anapata mashambulizi mengi ambayo huenda yangeonesha ubora wake kwa maana ya kuokoa lakini washambuliaji wa Simba walishindwa kufanya hivyo na kumfanya kuwa salama.

MICHAEL ISMAIL - 5

Alikuwa imara katika kutimiza vizuri majukumu yake ya kukaba na kuwazuia mawinga wa Simba, Ajibu, Kahata na Kanda ambaye aliingia kipindi cha pili.

Ismail alicheza vizuri na alihusika hata katika mashambuli ya Prisons kwa kupiga krosi na pasi kwa washambuliaji.

LAURIAN MPALILE - 4

Alitimiza vyema majukumu ya kukaba kama mpango ambao waliingia nao katika mechi ya jana, kwani hakuna mshambuliaji yeyote wa Simba aliyeweza kutumia upande wake wa kushoto kufanya shambulizi hatari.

VEDASTUS MWIHAMBI - 5

Mshambuliaji hatari kwa sasa hapa nchini ni Kagere kutokana na rekodi mbalimbali za kufunga ambazo ameweka lakini katika mechi ya jana Mwihambi alifanikiwa kufanya kazi kubwa ya kumkaba vyema na kumzuia asifanye madhara.

NURDIN CHONA - 5

Alicheza kwa maelewano makubwa na Mwihambi na kushirikiana kuokoa mipira mingi ya hatari ambayo ilikuwa ikienda kwa washambuliaji wa Simba Kagere, Chama na Shiboub. Chona mpaka mechi inamalizika alikuwa nguzo imara katika kikosi cha Prisons hasa katika nafasi ya ulinzi.

ADILLY BUHA - 6

Aliweza kutimiza majukumu ya ulinzi katika nafasi ya kiungo mkabaji ambayo alikuwa akicheza, pia alionesha uwezo katika kushambulia hasa akiwa na mpira na aliwazidi ujanja viungo wa Simba kina Mkude, Shiboub na Chama.

SALUMU KIMENYA - 5

Alicheza kama winga lakini hakuwa akifanya mashambulizi mengi ukiondoa shuti kali ambalo alipiga kipindi cha kwanza na kutoa, nje lakini muda mwingi alikuwa akimsaidia beki wa kulia Ismail katika kukaba.

EZEKIEL MWASHILINDI - 5

Alikuwa akicheza kama kiungo mshambuliaji lakini muda mwingi alikuwa hafanyi majukumu ya kushambulia, bali alikuwa akifanya majukumu ya kukaba na kuziba mianya ili timu yao isishambuliwe zaidi.

SAMSON MBANGULA - 4

Hakuwa anafanya mashambulizi mara kwa mara pengine kutokana timu na Prisons kuingi na mpango wa kujilinda zaidi na alijikuta muda mwingi akiwa mwenyewe pindi walipokuwa wakishambulia lakini Wawa na Nyoni wakifanikiwa pia kumzuia pindi alipokuwa na mipira.

ISMAIL AZIZI - 4

Alikuwa akicheza nyuma ya mshambuliaji lakini alikuwa akishuka katika eneo la kiungo kwani muda mwingi timu yao ilikuwa nyuma kuzuia mashambulizi ya wachezaji wa Simba ili wasilete madhara.

BENJAMINI ASUKILE - 4

Alikiwa akicheza kama winga wa kulia, lakini hakuonekana kufanya mashambulizi mara kwa mara kwenye lango la Simba.

Alicheza kwa mambo mawili kwanza kumsaidia beki wake wa kushoto na jambo la pili kuwasaidia viungo wa kati kukaba jambo ambalo alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kutibua mipango ya Simba.

Advertisement