Shilole, Lamar waomba kuuza chakula SGR

Muktasari:

Fursa zilizopo katika ujenzi wa reli ya umeme nchini, umewachanganya wasanii hadi wengine kufika hatua ya kuomba zabuni ya kuuza vyakula utakapokamilika.

Dar es Salaam. Msanii wa bongo fleva na filamu nchini, Zuwena Mohamed 'Shilole' pamoja na prodyuza Lamar, wameomba mradi wa treni ya umeme (SGR) utakapokamilika wapewe zabuni ya kuuza chakula.
Wametoa ombi hilo jana Alhamisi wakati wa ziara ya kutembelea mradi wa ujenzi wa treni hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro.
Wawili hao kwa pamoja wamewambia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Mkurugenzi wa Shirika la Reli (TRC) Masanja Kadogosa ambao walikuwa wameongozana na wasanii katika ziara hiyo iliyoishia kituo cha Ruvu.
Wasanii hao wamewaomba viongozi hao kumfikishia ombi lao, Rais John Magufuli na kueleza kuwa haitawasaidia wao tu bali kutoa ajira kwa wengine.
“Tunashukuru tumejionea maendeleo ya ujenzi wa reli hii na kwa maelezo tuliyoyapata ni wazi kwamba Watanzania na sisi tunatakiwa tuitumia treni hii katika kujitafutia kipato kama mlivyotambua mchango wetu katika kuangaza mradi huu, vivyo hivyo zinapotokea fursa msitusahau na sisi kwa kuwa tayari ni wajasiriamali,"alisema Shilole ambaye pia ni mmiliki  wa mgahawa wa Shishi Food.
"Tunaona idara ya chakula inatufaa kwa kuwa tumeianza muda mrefu sasa, naamini nitaitendea haki."
Kwa upande wake Lamar anayemiliki studio ya Fish Crab amesema naye anafanya shughuli hiyo japokuwa si wengi wanaojua.