Shikamkono: Hiki ndicho kilichotuponza kwa Stella Abidjan-5

Tuesday February 12 2019

 

By Mohammed Kuyunga

BADO tunaendelea na makala haya ya Jabir Ally Shikamkono yaliyofanyinyika kijijini kwake, Gomero, Kisaki mkoani Morogoro wiki iliyopita.

Tunaingia katika makala ya tano. Katika makala zilizopita, Shikamkono amefunguka mambo mengi yaliyojitokeza mwishoni mwa miaka ya 80 baada ya aliporudi kutoka Uarabuni.

Amezungumzia ufadhili wake ndani ya Simba, kuhusu kufilisika kwake kutokana na kuidhamini na kuifadhililabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam.

Pia, amefunguka kuhusu kuinusuru klabu hiyo isishuke daraja mwaka 1988 mbele ya watani wao wa jadi, Yanga na jinsi alivyofanya usajili wa wachezaji mbalimbali ndani ya klabu hiyo na visa na mikasa aliyokutana nayo.

Leo Shikamkono anafunguka kuhusu kile kilochotokea na kusababisha Simba kufungwa katika mchezo wa fainali wa Kombe la CAF (Sasa Kombe la Shirikisho) mwaka 1993 dhidi ya Stella Abijan jijini Dar es Salaam.

Simba ilianza safari yake ya kufika fainali ya Kombe la CAF baada ya kutoka sare tasa dhidi ya Ferreviaro de Maputo nyumbani na kwenda kutoa sare ya mabao ugenini (1-1).

Raundi ya kwanza ikaifunga Manzini Wonderers ya Swaziland (2-0) katika Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) na ugenini ikashinda 1-0. Ikaitoa Al Harrach ya Algeria kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya kushinda 3-0 nyumbani na kufungwa 2-0 ugenini.

Simba ikaifunga timu ngumu ya Atletico Aviacao (ASA) ya Angola mabao 3-1 nyumbani kisha ikaenda kupata sare tasa ugenini.

Shikamkono anaikumbuka mechi hii kwani ilikuwa na vituko vingi sana. Anasema Simba ilipewa ndege ya Waziri Mkuu, enzi hizo, John Samweli Malecela na kuondoka hadi Mwanza ambapo asubuhi wakati wakijiandaa kuondoka Uwanja wa Ndege wa Mwanza, ndege hiyo iligoma kuwaka.

“Ilikuwa patashika nguo kuchanika, ilibidi malori mawili yaje kuibusti ile ndege ili ipate moto,” anakumbuka Shikamkono.

Kitu kingine ambacho anakikumbuka katika mechi hiyo waliyoambatana na aliyekuwa kiongozi wa Simba, Mzee Amri Bamchawi ni jinsi mvua ilivyonyesha Angola baada ya miaka kadhaa.

“Brother mvua ilinyesha kuanzia saa tisa alasiri. Tena ilinyesha eneo la uwanja tu. Wenyeji walishangaa sana, kutokana na nchi ile kuwa na ardhi kame. Na kwa miaka miaka mingi mvua haikuwa imenyesha baada ya kufika sisi ikanyesha,” anasema.

Shikamkono anasema kipindi hicho hawakuwa na mchezaji hata mmoja wa kigeni, wote walikuwa wazawa.

Baada ya mchezo huo, Simba ikafanikiwa kucheza na Stella Abidjan na kutoka sare tasa kule Ivory Coast.

NINI KILITOKEA NYUMBANI?

“Si unawajua wachezaji wa Kitanzania? Walikuwa na asilimia mia kuwa tunashinda mchezo ule tulijaribu kuwaeleza lakini haikusaidia, waliridhika na kufanya mazoezi wanavyotaka,” anasema.

Mbali na kuridhika kwa wachezaji wa Simba baada ya kutoa sare tasa (0-0) ugenini staili ya Stella Abjan waliyokuja nayo nchini ilichangia. “Wale jamaa walifikia Hoteli ya Starlight pale Mnazi Mmoja wakajifungia ndani. Hawakufanya mazoezi wala nini hadi siku ya mechi ilipofika ndio wakatoka ndani ya kuja uwanjani. Wachezaji wetu kusikia hivyo wakaongeza ari ya kujiamini. Wakasema jamaa wamekata tamaa kuamini kuwa wanafungwa.

“Sio kweli kuwa tulihujumiwa au kuna mtu alihujumu timu, la hasha. Wenzetu walikuja na game plan nzuri, siye tulishindwa kupafomu. Pia, labda wacheaji walipagawa baada ya kuona Rais wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu na cabinet nzima ya mawaziri kuwapo uwanjani pale.

“Jamaa walipopata bao la kwanza wachezaji wetu walikuwa taabani. Walishachoka walivunjika nguvu na kila mmoja alikuwa akiomba kutoka uwanjani akisingizia kuumia. Tulikomaa na kuwambia hakuna kutoka hadi mechi iishe.”

AMGOMEA AZIM DEWJI TENA

Shikamkono anasema kabla ya mchezo huo, Mfadhili wa Simba wakati huo, Azim Dewji alipanga kuyaleta magari ya KIA uwanjani na kuyaweka kwenye geti la upande ule wa JKT lakini alimkatalia.

“Binafsi niliona kufanya hivyo ni kukufuru kabla hata hatujapata ushindi,” anakumbuka Shikamkono.

AMKUMBUKA JK

Baada ya Simba kufungwa, Dewji aliamua kuwapoza wachezaji wote wa Simba kwa kuwapa magari madogo aina ya Toyota Collora.

“Yale magari tuliomba tupunguziwe ushuru na serikali. Kuna mbunge alipinga sana lakini Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete (JK) wakati huo akiwa Waziri wa Fedha alitusaidia pamoja na U-Yanga wake,” anasema na kuangua kicheko.

APIGWA ZENGWE

Katika hatua nyingine, Shikamkono anakumbuka jinsi alivyopigwa zengwe baada ya kupewa uratibu wa timu hiyo na Dewji.

“Kuna watu hawakutaka miye niwepo Simba. Niliumia sana. Nilitumia pesa zangu kwa ajili ya timu kisha walewale uliokuwa ukiwaona ni wenzio wanakukataa, ilinichanganya sana,” anasema Shikamkono ambaye ni shabiki wa Liverpool katika Ligi Kuu England.

Baadhi ya wanachama na viongozi wa Simba walitaka Dewji asiwe anampa fedha za klabu, Shikamkono, bali fedha zote zipitie kwa mweka hazina wa klabu.

“Dewji aliwaambia huyu (Shikamkono) atanijibu mimi kama kutatokea ubadhilifu lakini mweka hazina ataujibu Mkutano Mkuu wa Simba na si mimi.”

Alhamisi Shikamkono atafunga kwa machungu yake kwa MO Dewji na kuhusu Hamis Gaga na Saidi Mwamba. Usikose.

Advertisement