Shikalo aipa Yanga siku saba

Muktasari:

Shikalo alisema anataka kutumia siku saba kupumzika na kuaga familia kabla ya kujiunga na Yanga, huku akisisitiza akili yake inawaza zaidi namna atakavyoanza maisha mapya Jangwani katika moja kati ya klabu kubwa na kongwe barani Afrika.

MAMBO yameiva huko Jangwani, baada ya kipa mpya wa timu huyo, Mkenya Farouk Shikalo kumaliza rasmi kazi ya kuitumikia Bandari Kenya kufuatia kutolewa ya michuano ya Kombe la Kagame 2019 yanayoendelea Rwanda, huku akiwapa mabosi wa Jangwani siku saba tu.

Kipa huyo amewaomba mabosi wake wampe siku hizo ambazo ni sawa na wiki moja, akiwa amerudi kwao Kenya kisha ndipo aje kuungana na timu hiyo kwa kambi ya mazoezi inayoendelea mjini Morogoro.

Akizungumza na Mwanaspoti, Shikalo alisema kwa sasa ameshamalizana na Bandari na yupo kwao Kenya kwa ajili ya mapumziko kwani hajapata wasaa huo kwa kuwa alikuwa Misri kwenye Afcon 2019 na Timu ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars na kuunganisha Kigali kwenye Kagame iliyoingia hatua ya robo fainali kwa sasa.

Alisema baada ya kutumia siku hizo chache kupumzika na kuweka mambo yake sawa kwao, ndipo atasafiri kuja Tanzania kuungana na wenzake kwa msimu mpya wa mashindano akiwa na kikosi hicho kwa mara ya kwanza tangu kilipomsajili akiwa Cairo, Misri.

“Nataka nipumzike kwa siku saba hapa nyumbani unajua sijapumzika kabisa, baada ya siku hizo nitakuwa Tanzania kujiunga na Yanga, kwani nimeshamaliza kazi Bandari,” alisema Shikalo ambaye ni kipa namba mbili wa Harambee Stars.

Shikalo alisema anataka kutumia siku saba kupumzika na kuaga familia kabla ya kujiunga na Yanga, huku akisisitiza akili yake inawaza zaidi namna atakavyoanza maisha mapya Jangwani katika moja kati ya klabu kubwa na kongwe barani Afrika.

Kipa huyo alisema juzi alitumia siku moja kuwaaga makocha, wachezaji wenzake na hata viongozi tayari kwa kuanza maisha mapya ndani ya Yanga.

“Akili yangu sasa inafikiria ni jinsi gani nitaanza kuitumikia Yanga kwa mafanikio, hii ni changamoto yangu mpya klabu inasubiria makubwa kutoka kwangu na sina wasiwasi na hilo juu ya ubora wangu muhimu ni kujipanga,” alisema kipa huyo atakayekutana na wenyeji wake, Klaus Kindoki na mgeni mwenzake Mechata Mnata kutoka Mbao FC.

Shikalo ni kati ya wachezaji wapya 13 waliosajiliwa na Yanga msimu huu ambao wanaunda kikosi cha nyota 29 watakaoiwakilisha timu hiyo katika Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la FA, Kombe la Mapinduzi na michuano mingine itakayoshiriki msimu huu.