Shafiq Bantambuze atua Gor Mahia

Muktasari:

Shafiq Bantambuze, ambaye ni beki wa kulia, anakua nyota wa kwanza kusajiliwa na mabingwa hao mara 17 wa KPL, ambapo akitokea Singida FC ya Tanzania, ambapo anatajwa kuwa mrithi wa Godfrey Walusimbi, ambaye ametimkia katika klabu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Nairobi, Kenya. Siku moja baada ya ratiba ya msimu wa 2018/19 ya ligi kuu ya Kenya (KPL), kuwekwa hadharani, Mabngwa watetezi wa KPL, klabu ya Gor Mahia, imetangaza kuipata saini ya beki wa klabu ya Singida FC ya Tanzania, Mganda Shafiq Bantambuze.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo va habari, iliyotolewa rasmi kwenye mtandao wa klabu hiyo ni kwamba, Bantambuze ambaye anatajwa kuwa mrithi wa Mganda mwenzake, Godfrey Walusimbi, aliyetimkia katika klabu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, amejifunga na Kogalo kwa mkataba wa miaka miwili.
Nyota huyo wa zamani wa klabu ya  Tusker FC, ametua wakati ambapo mabingwa hao mara 17 wa soka nchini, wakijiandaa na msimu mpya wa Ligi ambapo Desemba 8, wataanza kampeni ya kutetea taji lao dhidi ya Bandari FC, ugani Mbaraki, Mjini Mombasa.
Gor Mahia ambao wataliwakilisha taifa katika michuano ya klabu bingwa Afrika, wako katika maandalizi ya kucheza mechi ya kirafiki na klabu ya Everton FC ya Uingereza, ambayo inatarajiwa kupigwa Novemba 6, mwaka huu, ugani Goodison Park, mjini Liverpool, Uingereza.
Wakati Batambuze akithibitishwa kuwa mchezaji halali wa Gor Mahia, kuna taarifa kuwa kiungo wa zamani wa klabu hiyo, Kenneth Muguna, ambaye kwa sasa ameachana na klabu ya KF Tirana ya Albania, aliyojiunga nayo mwanzoni mwa mwaka huu, yuko mbioni kutua Kogalo.
Inadaiwa kuwa Muguna ambaye aliwahi kuwa mchezaji bora wa mwaka (2015/16), anakaribia kutua klabuni hapo, hii ikiwa ni kwa mara ya pili, kwani itakumbukwa kuwa, baada ya kuonesha uwezo mkubwa na Western Stima, Muguna aliamua kujiunga na Kogalo, akaitumikia kwa msimu mmoja kabla ya kutimkia Albania.
Aidha, taarifa z uhakika zilizoifikia Mwanaspoti Digital, zinasema kwamba Gor Mahia, ina mpango wa kuvamia ngome za klabu ya Sofapaka kwa ajili ya sajili ya Kiungo wa klabu hiyo na Harambee Stars, Dennis Odhiambo.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa Kogalo tayari wameshatuma mshushushu wao klabuni hapo, kufuatilia nyendo za kiungo huyo wa zamani wa Thika United na ikiwezekana kuulizia kuhusu uwezekano wa kuipata saini yake, kwa ajili ya msimu ujao wa KPL.