Shabiki wa Real Madrid akunwa na bao la Messi

Muktasari:

Ni shuti la maana lililozaa bao ambalo alilishangilia kwa kukimbia katika eneo la mashabiki wa Barca, kama vile akiwataka kutulia, akiiga staili ambayo Raul, mshambuliaji wa zamani wa Real Madrid aliwahi kuifanya.

KATIKA toleo lililopita mwandishi Luca Caioli alilichambua bao zuri la Ronaldo lililoisambaratisha Barca nyumbani kwao Nou Camp na kuwa sababu ya kuipa Real Madrid taji la Ligi Kuu Hispania au La Liga. Sasa endelea…

Ni shuti la maana lililozaa bao ambalo alilishangilia kwa kukimbia katika eneo la mashabiki wa Barca, kama vile akiwataka kutulia, akiiga staili ambayo Raul, mshambuliaji wa zamani wa Real Madrid aliwahi kuifanya.

“Tulieni tulieni, niko hapa,’’ alisema kwa sauti ya juu, akiwa anajua nini maana ya bao hilo.

Katika mkutano na waandishi wa habari baada ya mechi hiyo Ronaldo alisema :“Ni bao muhimu lakini ushindi wa timu kwa jumla ni kitu muhimu.” Alikuwa amefunga bao kwa mara nyingine Nou Camp, akifanya kazi yenye manufaa iliyofuta ukame wa miaka mitatu kwa timu yake.

Na kwa namna vyombo vya habari vya Madrid vilivyolichukulia tukio hilo, ilikuwa kama vile Ronaldo alimbwaga Messi.

Messi: Barca v

Bayern Munich

Hii ni mechi ya hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyopigwa, Mei 6, 2015 wakati huo kocha wake wa zamani Pep Guardiola tayari alikuwa ameshaondoka Barca muda mrefu na katika mechi hiyo alikuwa akiinoa Bayern, vigogo wengine wa soka la Ulaya.

“Mabao haya ya kipekee yanatukumbusha kwa mara nyingine kwamba yeye ndiye bora, anapokuwa uwanjani tunakuwa tumejihakikishia ushindi,” hayo ni maneno ya kiungo wa Barca Andres Iniesta ambaye kimsingi anamzungumzia Messi.

Messi alikuwa ametoka kufunga bao muhimu la nusu fainali dhidi ya Bayern iliyokuwa chini ya Pep ambaye wakati akiwa Barca, Messi alifurahia kipindi kizuri cha mafanikio ya maisha yake ya soka.

Si tu kwamba alicheza akiwa mfano wa ‘stelingi’ wa filamu, bali pia alifunga moja kati ya mabao matamu lililopata kura na kuwa bao bora la mashindano hayo msimu wa 2014/15. Kura hizo zilipatikana kwa njia ya mtandao kupitia gazeti la michezo la Marca.

U-‘genius’ wake ulionekana katika kipindi cha pili, ubao wa matokeo ulisomeka 0-0 hadi katika dakika ya 77, baadaye Dani Alves aliunasa mpira katika wingi ya kulia na kumpasia Messi ambaye alifumua shuti kali nje ya boksi. 1-0, lakini hilo halikuwa bao lenyewe lililokuwa gumzo zaidi.

Dakika tatu baadaye, aliunasa mpira na kukutana ana kwa ana na Jerome Boateng na kumzunguka kwa umaridadi wa hali ya juu kiasi kwamba beki huyo akajikuta akikosa umakini wake uliozoeleka na kuanguka chini.

Messi akaendelea na kasi yake kabla ya kuupiga tena mpira kiufundi kwa staili kama vile kuudokoa, mpira ulikwenda juu na kumzidi kipa Manuel Neuer. Bao la ukweli, bao la maana.

Wachezaji wenzake walimkimbilia na kumzunguka, mashabiki waliojazana kwenye Uwanja wa Nou Camp nao walilipuka kwa shangwe. Mechi hiyo ilimalizika kwa Barca kutoka na ushindi wa 3-0. Bao la tatu la Barca lilifungwa na Neymar.

“Ni kweli mambo yanakuwa rahisi Messi akiwa uwanjani, anaweza kufanya lolote, tunakumbushwa kila siku kwamba huyu ni wa aina yake,” alisema Kocha wa Barca Luis Enrique ambaye katika msimu huo alikuwa na matatizo ya hapa na pale na Messi.

Hata mashabiki wa mahasimu wao Real Madrid au baadhi ya mashabiki hao walilikubali bao hilo kwamba ni la kipekee, “Namvulia kofia Messi,’’ alisema katika mtandao wa Twitter bingwa mara mbili wa mbio za magari za Dakar Rally ambaye pia ni shabiki wa kutupwa wa Real Madrid, Carlos Sainz.

Na Messi mwenyewe akizungumzia bao hilo alisema, “Ni tukio zuri katika kuelekea kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya nne.”

Itaendelea Jumanne ijayo…