Sh170 milioni kuipeleka Mbeya Kwanza VPL

LIGI Daraja la Kwanza (FDL) inatarajia kuanza Oktoba 9, mwaka huu ambapo kuna makundi mawili yenye timu 10 kila kundi.

Mbeya Kwanza ipo Kundi A pamoja na timu za African Lyon, Ndanda FC, Majimaji FC, Njombe Mji, Gipco FC, Boma FC, Mawenzi Market FC na Lipuli FC.

Timu hiyo ambayo imepambana kupanda Ligi Kuu Bara kwa misimu mitano itakutana na timu mbili zilizoshuka daraja msimu uliopita ambazo ni Lipuli FC ya mjini Iringa na Ndanda FC ya Mtwara.

Msimu uliopita timu zingine kama Majimaji, Njombe Mji, Gipco, Boma na Mawenzi Market hazitakuwa ngeni kwa Mbeya Kwanza kwani ni miongoni mwa timu zinazopambana kupanda daraja kwa misimu mingi, hivyo watakapokutana hawataonana kuwa wageni.

Mbeya Kwanza yenye maskani yake maeneo ya Iyunga, Mbeya Mjini iliingia kambini mwezi mmoja uliopita yote hiyo ni kujiimarisha kwa ajili ya kusaka pointi zitakazowawezesha kupanda ligi kuu.

Msimu uliopita timu hiyo ilishika nafasi ya nne ikiwa na pointi na 37 wakiwa Kundi A pamoja na Ihefu na Dodoma Jiji ambazo zilipanda Ligi Kuu.

Makala haya inakuletea namna ambavyo timu hiyo imejiandaa kuwania kupanda Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Mohamed Mashango anasema kuwa kila msimu wanajipanga lakini ushindani wanaokutana nao ndiyo unaowarudisha nyuma ingawa msimu huu malengo na matumaini ni makubwa mno.

BAJETI

Kuna baadhi ya timu za FDL hazina bajeti kabisa kutokana na ukata unaozikabili, hivyo bajeti yao hutokea tu pale wanapokuwa na mechi na si kama ilivyo kwa Mbeya Kwanza ambao bajeti yao ya msimu inajulikana.

Mashango anasema ili wafanye vizuri uongozi wake umeandaa bajeti ya Sh170 milioni kwa msimu mzima.

“Hiyo ni kila kitu kuanzia maandalizi, mishahara ya wafanyakazi wote wa timu, kwetu ni bajeti kubwa kulingana na mazingira ya ligi yenyewe, ingawa sasa hivi angalau kuna udhamini kidogo lakini tunapaswa kupambana zaidi. FDL ni ligi ngumu na inahitaji maandalizi makubwa,” anasema Mashango.

KAMBI

“Timu ilikuwa kambini kwa zaidi ya mwezi mzima, vijana wapo tayari, kundi letu tunaona ni gumu sababu timu zote zinajiandaa kulingana kila mmoja wetu kutaka kupanda, tofauti ipo sababu kuna timu tulicheza nazo ila safari tumepata timu mpya mbili zimetoka Ligi Kuu,” anasema.

“kwa hiyo zitatupa changamoto kubwa sana, ili tufanye vizuri zaidi, msimu uliopita tulikosea sehemu ndogo sana sababu kuu mechi hizi za FDL lazima uwe umejipanga vizuri zaidi, naamini msimu huu tutafanya vizuri zaidi ya msimu uliopita, unavyojiandaa na mwenzio anajiandaa hivyohivyo, ndio sababu tukafanya vibaya baadhi ya mechi ila safari hii tutafanya vizuri.”

USAJILI

Mbeya Kwanza imesajili wachezaji 26 huku mchezaji mkongwe ndani ya kikosi hicho akiwa ni mmoja tu David Naftal ingawa msimu uliopita alikuwepo pia Danny Mrwanda.

“Usajili wetu ni mkubwa zaidi ya msimu uliopita na tunaamini tutafanya vizuri sana, matarajio yetu tuvuke na kupanda msimu huu mpya unaoanza, wachezaji wengi wale wale tuliokuwa nao msimu uliopita sababu tunaamini watafanya vizuri kwa kuzoweana kwao tangu msimu uliopita,” anasema.

CHANGAMOTO

Mashango anasema kuna changamoto nyingi wanakabiliana nazo kwenye hiyo, lakini kubwa amewaomba na kuwakumbusha waamuzi kuchezesha kwa kufuata sheria na kanuni za soka ili kumpata mshindi kihalali.

“Changamoto zipo nyingi sana kwenye FDL na hii yote inatokana na timu kutokuwa na udhamini, lakini kikubwa ni kuwakumbusha waamuzi kuchezesha kwa kufauta sheria za soka.

“Miaka ya sasa hakuna malalamiko mengi sana ila ni kukumbushana tu juu ya waamuzi kuongeza umakini ili ligi iwe na ushindani, mvuto na kumpata mshindi pasipo malalamiko,” anasema Mashango.

MECHI YA UFUNGUZI

Kuhusu mechi yao ya ufunguzi wa ligi hiyo ambapo Mbeya Kwanza inaanzia ugenini, Mashango anasema; “Hakuna mechi rahisi kwenye ligi yeyote hata huku FDL ndiyo kugumu zaidi ila tunajipanga kuhakikisha tunashinda hata ugenini, tunafahamu hata wao wamejipanga ila nasi tunajipanga,”.

Mbeya Kwanza ambayo ipo chini ya kocha mkuu Steven Matata inaanza kucheza na Njombe Mji, Oktoba 10, 2020 kwenye Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe.

Ligi hiyo inashirikisha timu 20 zitakazochuana kusaka timu za kupanda na kushuka Daraja la Pili msimu ujao.