Sevilla wampaisha Mendy Chelsea

Muktasari:

Kiwango ambacho amekionyesha Edouard Mendy kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Sevilla kimeendelea kumhakikishia namba ya kucheza kikosi cha kwanza cha timu hiyo mbele ya Kepa Arrizabalaga.

LONDON, ENGLAND. KOCHA wa Chelsea, Frank Lampard amesema kiwango ambacho amekionyesha Edouard Mendy kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Sevilla ambao ulimalizika kwa suluhu kimethibitisha kuwa yeye ni golikipa chaguo la kwanza wa kikosi hicho.

 

Mendy, ambaye alijiunga na Chelsea akitokea Rennes ya Ufaransa, alionyesha kiwango kikubwa kwenye mchezo huo wa kwanza wa 'The Blues' ambao walikuwa nyumbani kwenye uwanja wao wa Stamford Bridge.

 

Katika mchezo huo, kipa huyo raia wa Senegal aliokoa michomo miwili ya hatari ambayo ingeiweka pabaya Chelsea, miongoni mwa hatari hizo ni pamoja na ile ambayo Nemanja Gudelj alipiga kichwa ambacho kilimgonga Kurt Zouma.

 

Mpira ule ulibadili uelekeo baada ya kumgonga Zouma ambaye kwenye idara ya ulinzi wa kati Chelsea alicheza na mkongwe, Thiago Silva lakini Mendy kwa haraka naye akaufuata na kuondoa hatari.

 

Alipoulizwa kuwa hivi Mendy ni tayari chaguo lako la kwanza? Lampard amesema, "Kwa sasa ndio. Ameonyesha ubora wake. Vile ambavyo amekuwa akicheza amekuwa akifanya vizuri, hajaruhusu bao kwenye michezo yake miwili hadi sasa, anasimama kama namba moja."

 

Suluhu ambayo Chelsea imetoka dhidi ya Sevilla ni ya kwanza chini ya Lampard, The Blues walicheza vizuri kwenye idara yao ya ulinzi tofauti na namna ambavyo wamekuwa wakicheza kwenye michezo yao iliyopita.

 

Zouma na Ben Chilwell wote walipoteza nafasi za kuifungia mabao Chelsea hapo jana baada ya vichwa ambavyo walipiga wakiwa huru kudakwa kirahisi na mlindalango wa Sevilla,Yassine Bounou.

 

Wakati matokeo yakiwa hivyo kwa Chelsea na Sevilla, wapinzani wao kwenye kundi E nao walishindwa kutambiana, Rennes ya Ufaransa walitoka sare bao 1-1 dhidi ya Krasnodar ya Russia.

 

MATOKEO KWA UJUMLA

 

Chelsea 0 - 0 Sevilla

Rennes 1 - 1 FC Krasnodar

Zenit 1 - 2 Club Brugge

Lazio 3 - 1 Borussia Dortmund

Dynamo Kyiv 0 - 2 Juventus

Barcelona 5 - 1 Ferencvaros

PSG 1 - 2 Man United

Leipzig 2 - 0 Istanbul Basaksehir