Serikali yaikubali kampeni ya Mo Dewji

Muktasari:

Kutokana na Uwanja wa Taifa kutumika katika shughuli mbalimbali na kuingiza watu wengi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohammed Dewji, amemuomba Rais, John Magufuli kubadilisha jina uitwe William Benjamin Mkapa.

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Mohammed Dewji 'Mo Dewji', amemuomba Rais, John Pombe Magufuli kubadilisha jina la Uwanja wa Taifa, kuitwa Benjamin William Mkapa.

Katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Mo Dewji alindika kuwa "Leo nimeamua kuanzisha petition (maombi) kwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Pombe Magufuli kubadili jina la Uwanja wa Taifa kuwa: Uwanja wa Benjamin William Mkapa"

Ameendelea kuelezea kuwa ujenzi wa Uwanja wa Taifa, ulianzishwa na Rais wa awamu ya tatu, Mkapa ambapo una uwezo  wa kubeba mashabiki 60,000  na ni miongoni mwa viwanja bora katika bara la Afrika kwa sasa.

"Uwanja huo kwa namna mmoja au nyingine, umesaidia kuendeleza mpira wa miguu na michezo mingine nchini Tanzania, uzuri na ukubwa wa soka letu umedhihirishwa kwa sababu ya uwanja wetu huo ambao unashika nafasi ya 11 kwa ukubwa Afrika,"ameandika Mo Dewji.

Amesema uwanja huo wa kisasa umeongeza uzalendo mkubwa kwa kuwezesha maelfu ya mashabiki kuwa sehemu ya michezo mikubwa, pia umeongezea mapato kwa klabu na kuleta heshima kubwa nchini kwamba mifano ipo dhahiri.

"Kutokana na uzuri wa uwanja huo, klabu za nje ambazo zinakuja kucheza katika uwanja huo, zimekuwa zikitoa sifa mbalimbali, timu za mataifa makubwa kama Brazil zimecheza kwenye uwanja huo na kumwaga sifa nyingi,"

Ameongeza kuwa "Nje na michezo uwanja huo, umetumika kufanyia mashindano ya usomaji wa Quran, mashindano makubwa ya kusoma Quran barani Afrika ambayo yanamkusanyiko mkubwa, hii nayo ilikuwa ni rekodi nzuri kwetu Watanzania,"

Amesema wameshuhudia matamasha mbalimbali makubwa kama matamasha ya Pasaka na Krsimasi yakifanyika uwanja huo na lengo la yote hayo ni kuleta umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania.

"Itakuwa ni heshima kubwa kama uwanja wetu pendwa utaitwa jina la Uwanja wa Benjamin William Mkapa, tunamuomba Rais John Pombe Magufuli aridhie kubadili jina la uwanja huo, kwa heshima ya Hayati Mkapa ili tuendelee kumkumbuka kwa mchango wake mkubwa na hasa kwa vizazi vijavyo,"amesema.

Amewaomba Watanzania wote bila kujali ushabiki wa klabu, kuunga mkono kwa kuweka sahihi ili wamuombe Rais kubadilisha jina la uwanja huo uitwe Benjamin William Mkapa Stadium au Uwanja wa Benjamin William Mkapa.

 

Akijibu kuhusu kampeni hiyo Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas amesema hoja hiyo iliyotolewa na Mo Dewji kutaka Uwanja ubadilishwe jina na kuitwa Benjamin William Mkapa ni nzuri.

“Hoja nzuri tutaichukua kama unavyofahamu historia yake ulijengwa kwa jitihada zake kwahiyo hili ni jambo tunamshukuru kwenye sekta ya michezo na wala sioni kama lina mjadala acha tumalize mazishi kisha tutasikiliza hoja hiyo ya wadau” amesema Abbas ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo