Serengeti Boys yaipa mchecheto Nigeria

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa mtandao wa Allnigeriasoccer.com, katika kundi hilo la zaidi ya wachezaji 400 ambalo lipo chini ya kocha mkuu, Manu Garba amewaita pia wachezaji wanne wanaocheza soka barani Ulaya.

HOMA ya mashindano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 imeanza kupamba moto kwa timu ya taifa ya vijana ya Nigeria ‘Golden Eaglets’ imekusanya wachezaji zaidi ya 400 ambao itawafanyia mchujo na kubaki 21 tu ambao itawatumia kwenye mashindano hayo.

Katika mashindano hayo, Nigeria imepangwa kundi moja sambamba na wenyeji Tanzania ‘Serengeti Boys’, Uganda ‘Uganda Cubs’ na Angola ‘Os Palanquinhas.

Kwa mujibu wa mtandao wa Allnigeriasoccer.com, katika kundi hilo la zaidi ya wachezaji 400 ambalo lipo chini ya kocha mkuu, Manu Garba amewaita pia wachezaji wanne wanaocheza soka barani Ulaya.

Kipa Joseph Oluwabusola anayedakia Bournemouth ya England, Kelechukwu Ebenezer Ibe-Torti anayechezea Barcelona, mshambuliaji wa Go Ahead Eagles ya Uholanzi Lateef Omidiji pamoja na nyota mwingine anayecheza Canada ambao watapimwa viwango vyao kupitia mchujo huo.

Hata hivyo hadi sasa kipa oluwabusola ameshindwa kuhudhuria mchujo huo kutokana na kubanwa na ratiba ya mitihani hukos nchini England.