Serengeti Boys kwenda kujifua Qatar

Thursday March 14 2019

 

By Majuto Omary

Dar es Salaam. Timu ya Taifa ya vijana Serengeti Boys inatarajiwa kuondoka nchini Machi 20 kwenda Doha, Qatar kwa ajili ya kambi ya mwisho kabla ya kushiriki mashindano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) yaliyopangwa kuanza Aprili 14 mpaka 28 jijini Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo alisema kambi hiyo itawasaidia wao kunoa makali ya wachezaji wake kabla ya kuanza kwa mashindano hayo mwezi ujao.

Hivi karibuni Serengeti Boys ilishiriki katika mashindano maalum yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa Assist) yaliyofanyika mjini, Antalya, Uturuki na kucheza mechi tatu.

Timu hiyo ilianza kwa kufungwa bao 1-0 na Guinea kabla ya kupata ushindi wa 3-2 dhidi ya Australia na baadaye kupoteza kwa mabao 5-0 dhidi ya wenyeji Uturuki.

Pamoja na matokeo hayo, mashindano hayo yaliwapa fursa kubwa wachezaji wa Serengeti Boys kunoa na kurekebisha makosa yao kabla ya kuanza kwa mashindano hayo.

Alisema kuwa mbali ya kucheza mechi dhidi ya wenyeji, pia timu hiyo itacheza mechi za kujipima nguvu dhidi ya timu mbalimbali kutoka mataifa ya karibu na Qatar.

Advertisement

“Kambi hii itatoa fursa kwa wachezaji kujiandaa zaidi baada ya mashindano ya Uturuki. Wachezaji wanaendelea vizuri na mazoezi hapa nchini na kwa kifupi wameiva na wapo tayari kwa ajili ya mashindano.

“Kinachofanyika ni kunoa makali yao zaidi na huku tukirekebisha makosa yaliyoonekana katika mechi zilizopita, tumejifunza mengi sana Antalya na kubwa zaidi, morali ya wachezaji ipo juu na wana kiu ya kufanya vizuri,” alisema Mirambo.

Serengeti Boys ipo katika Kundi A pamoja na Nigeria Angola na Uganda, huku Kundi B lina timu za Guinea, Cameroon, Morocco na Senegal.

Serengeti Boys itaanza kampeni za kutwaa ubingwa wa Afcon dhidi ya Nigeria Aprili 14 kabla ya kupambana na Angola Aprili 17 na mechi ya mwisho kumaliza na Uganda.

 

Advertisement