Senzo apania mechi ya watani-3

Wednesday October 28 2020
senzo pic

TUMEINGIA sehemu ya mwisho ya mahojiano yetu na Mshauri wa uongozi wa Yanga, Senzo Mazingisa na kwenye toleo lililopita alielezea ujio wa kocha mpya ndani ya kikosi hicho, Cedric Kaze na yale aliyopanga kuyafanya.

Kigogo huyo anaendelea kusema: “Kufanya kazi nje ya kwetu ni moja ya fursa kubwa niliyoitumia kujijenga. Nimepata uzoefu mkubwa sana kwa muda ambao nimefanya kazi hapa Tanzania. Ni hatua kubwa sana nimepiga katika maisha yangu ya ajira. Nguvu ya siasa za soka hapa zimenifunza mengi sana.”

“Pia nimekuwa imara sana na nafaidika pakubwa. Najua jinsi ya kuweka mizani sawa juu ya siasa na mpira na natambua mimi ni raia wa kigeni na jinsi ya kuishi sehemu yoyote.

“Hapa Tanzania maisha yamekuwa tofauti. Presha ni kubwa lakini sasa najua jinsi ya kufanya kazi nikiwa kwenye presha kubwa. Kila wakati uko kwenye presha hakuna nafasi ya kutulia na kama ipo inakuwa kwa kiasi kidogo sana, sasa mimi kama Senzo hicho ndicho napenda na najiona kama niko katika wakati sahihi katika mazingira hayo magumu.

“Kuna watu wanaweza kujiuliza nawezaje kufanya kazi katika nchi ambayo ipo chini kisoka. Ndio, kwangu ni nzuri. Wanatakiwa waje ili wajue kukoje. Pia napenda kujifunza jinsi serikali ya hapa ilivyo karibu na mambo ya soka, nchi zingine hili sio rahisi sana kuliona. Nimejifunza mengi sana katika kufanya kazi na watu wa serikali kwa ukaribu na bila kuona migongano.

“Mfano mzuri ni hapa kati lilipotokea janga la Covid 19, hii imenipa uzoefu wa kutosha, nafikiri naweza kuwa raia pekee wa Afrika Kusini aliye nje ya taifa lake akifanya kazi wakati wa janga lile, labda sasa naweza kuungana na kaka yangu Pitso Mosimane (Kocha wa Al Ahly ya Misri).”

Advertisement

SIMBA, YANGA WANAKWAMA WAPI?

“Kikubwa ni pesa, muundo wa uongozi bora wa kisasa kuhusu soka na uwekezaji. Huwezi kushindana na klabu ambayo inanunua mchezaji mmoja kwa bilioni 3, hapo hatujaweka mishahara, halafu ukailinganisha na klabu ambayo inasajili mchezaji mmoja kwa Dola 60,000 kwa miaka miwili, haiwezi kuwa rahisi, klabu za hapa bado zina safari ndefu sana ya kufikia huko.

“Binafsi nawapongeza TFF kwa akili ya uwekezaji wanaotaka kuufanya kupitia hii miradi ya Fifa katika kujenga vituo ya soka. Hilo pekee linaonyesha kuna safari Tanzania mnaanza kuipiga hapa katika kukuza soka na litasaidia kuitangaza nchi duniani, sasa mna nia ya kutaka kufika mbali kimaendeleo.

“Nafikiri hapo ndipo klabu hizi zinapoachwa na hizi klabu kubwa Afrika. Mfano mzuri ni Mamelodi Sundowns, wanalipa vizuri mpaka unaweza kuchanganyikiwa. Ukilinganisha na malipo ya hapa utagundua bado kuna tofauti kubwa sana. Sisemi pesa pekee ndio inaweka tofauti, lakini unapokuwa na pesa utamsajili yeyote unayemtaka, utaweka miundombinu mizuri na ya kisasa zaidi.

“Hata hivyo, Tanzania na hasa mfano mzuri klabu yangu Yanga, kuna hiyo nafasi. Hata hivyo, kwa sasa tujenge tunachokipigania kubadilisha mfumo wa uongozi wa klabu, tujiweke katika mazingira ambayo tunaweza kufanya biashara ya mpira na kuwavutia watu, tuwajengee mashabiki na wanachama, kama uongozi ukisema unataka kujenga idara yao kubwa ya kisasa ya mawasiliano wanaamini na hapa wengi watakuja kuweka pesa kwa sababu hata wao wanatamani kuona klabu inapiga hatua kubwa kimaendeleo. Najua itachukua muda na sio rahisi lakini inawezekana hata hizo klabu kama TP Mazembe zimeanzia mbali.

USAJILI WA MORRISON

“Moja ya kitu ambacho huwa kinanipa raha katika soka la Tanzania, ni uvumi kila unapopita, utasikia kuhusu hili au lile, kusema ukweli halikuwa jambo ambalo kama limepangwa, imetokea tu yeye anakwenda Simba na mimi nakuja Yanga, unajua klabu hizi zinajiendesha katika mazingira tofauti.

“Siwezi kusema nilikuwa sehemu ya mazungumzo ya usajili wa Morrison, sikuhusika na majadiliano ya usajili, kuna wakati nilijua klabu ilikuwa inataka kumsajili Morrison kwa kuwa kule wana kamati ya usajili kwa hiyo kama mtendaji nilikuja kusikia baadaye na haikuwa rasmi sana, lakini nilijua sio kila mchezaji anayesajiliwa nilikuwa na nafasi ya kujua.

“Nakumbuka wakati nakaribia kuondoka ndio nilisikia kuna huo mpango wa kutaka kumsajili na kwenye jambo ambalo sijashirikishwa huwa sisumbuki kutaka kujua sana ingawa sitaki kuongea sana.

TOFAUTI YA YANGA NA SIMBA

“Simba wako juu kwa kuwa Mohamed Dewji ana maamuzi ya kutaka kufanya lolote katika kuipeleka Simba mbele na Yanga watakuwa nyuma kwa kuwa bado hawajafikia mwafaka kwenye kubadilisha mfumo wa uendeshaji, kitu ambacho wanakifanya sasa hata kama zipo changamoto katika mfumo wao. Tayari Simba wameshatoka hapo, muhimu sasa ni Yanga nao kuangalia uharaka wa kutoka hapa ili mambo yaweze kwenda kisasa zaidi.

“Unajua Yanga ni klabu ya wananchi, ni hatua nzuri lakini kuna maeneo lazima yaimarishwe yaweze kuendana na mazingira ya kisasa. Ni wakati sasa watu kuendelea kupambana usiku na mchana kuhakikisha mabadiliko haya yanafanikiwa na kuipa hadhi klabu hii.

“Kwa hiyo kwa sasa ni ngumu kuzilinganisha klabu hizi mbili kwa kuwa klabu moja ilianza haraka na ikaondoka ilipokuwa.

“Nimesaini mkataba wa miezi 18 na Yanga ambao ndani yake kuna uwezekano wa kuongeza zaidi kama wahusika wa klabu wataona kuna hatua ya kimaendeleo katika ufanisi wa kazi, binafsi napenda mkataba wa namna hii kwa kuwa unatoa nafasi ya mimi kufanya kazi kwa nguvu, pia unatoa nafasi hawa pia ninaofanya nao kazi kunipa nafasi ya kutekeleza yale ambayo taaluma yangu inaniambia natakiwa kuyafanya kusaidia klabu.

PRESHA YA MECHI YA WATANI

“Hii ni mechi kubwa sana hapa lakini kama ninavyosema huwa napenda kufanya kazi katika mazingira ya presha. Naamini ndio hunijenga zaidi. Najua mechi iliyopita Yanga tulipoteza kwa mabao 4-1 nakumbuka kabla ya mechi presha ilikuwa kubwa sana kule Simba, lakini naamini sasa mechi ijayo nitakuwa huku Mungu akipenda na ninavyoona presha itakuwa kubwa mara mbili yake kwangu.”

 

Advertisement