Sarri akitemwa tu watu wanambeba

Muktasari:

  • Sarri atarudi kwenye soka la Italia ikiwa ni mwaka mmoja tu kupita tangu alipoondoshwa Napoli na kwenda huko Chelsea. Lakini, hilo kama Chelsea wataamua kuachana naye mwishoni mwa msimu huu.

ROME, ITALIA.KOCHA wa Chelsea, Maurizio Sarri ametajwa kushika namba moja kwenye orodha ya watu wanaosakwa na AS Roma ili akachukue mikoba ya kuinoa timu hiyo msimu ujao.

Sarri maisha yake huko Stamford Bridge yamekuwa kwenye mashaka makubwa baada ya timu yake kupita kwenye vipindi vizito katika huu msimu wake wa kwanza kabisa huko kwenye Ligi Kuu England.

Sarri ameshindwa kujikusanyia mashabiki kutokana na staili yake ya soka analofundisha, lakini kikosi chake cha Chelsea bado kipo kwenye nafasi nzuri ya kuwapo kwenye Top Four ya Ligi Kuu England huku jana usiku leo Alhamisi walitarajia kuwa mzigoni kwenye robo fainali ya Europa League. AS Roma wanahitaji huduma ya kocha huyo ili kuwafanya kuwa na nguvu kwenye mchakamchaka wa kulibeba taji la Serie A.

Sarri atarudi kwenye soka la Italia ikiwa ni mwaka mmoja tu kupita tangu alipoondoshwa Napoli na kwenda huko Chelsea. Lakini, hilo kama Chelsea wataamua kuachana naye mwishoni mwa msimu huu.

Roma ilihitaji huduma ya kocha Antonio Conte, aliyewahi kuinoa pia Chelsea, lakini wakaamua kumpa kazi Claudio Ranieri kwa muda hadi mwisho wa msimu. Tangu Februari kumekuwa na taarifa hizo za Sarri na kuelezwa kwamba ameshakutana na mabosi wa AS Roma na kwamba wanachosubiri ni Chelsea tu wamfute kazi ili wao wafunguke rasmi.