Sarri afutwa kazi Juventus

TURIN, ITALIA
JUVENTUS imemfuta kazi Kocha Maurizio Sarri, huku tayari ikimuoroshesha meneja wa zamani wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino kwenye orodha ya mabosi wapya wanaofikiriwa kupewa mikoba ya kuinoa timu hiyo.
Kocha huyo Mtaliano, Sarri mwenye umri wa miaka 61 amefunguliwa mlango wa kutokea siku moja tu baada ya Juventus kutupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na miamba ya Ufaransa, Lyon.
Sarri, alijiunga na Juventus akitokea Chelsea mwaka mmoja uliopita, akiwa na miamba hiyo ya Turin, ameshinda ubingwa wa Serie A msimu huu, lakini kufeli kwenye michuano ya Ulaya kumefanya kibarua chake kuota nyasi.
Kwa mujibu wa Sportitalia, miamba hiyo ya Turin inamtaka Pochettino atue Allianz Stadium.
Kocha huyo wa zamani wa Tottenham kwa sasa hana timu tangu alipofutwa kazi huko London, Novemba mwaka jana.
Ripoti zinadai kwamba Juventus imeshafanya mazungumzo na Muargentina huyo juu ya kwenda kumpa kibarua hicho.
Rais wa Juventus, Andrea Agnelli chaguo lake la kwanza la kumbadili Sarri ni Zinedine Zidane, ambaye pia timu yake ya Real Madrid ilitupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya usiku wa Ijumaa.
Kocha wa Lazio, Simone Inzaghi ni jina jingine linalopewa nafasi huko Turin, lakini makocha hao wawili wote wana ajira zao kwa sasa, isipokuwa Pochettino, ambaye ndiye mwenye nafasi kubwa ya kunasa kirahisi.