Sanchez anapiga pesa tamu akiwa tu benchi

Muktasari:

  • Amefunga mabao matano tu katika mechi 41 alizoichezea timu hiyo kwenye michuano yote na huenda akafunguliwa mlango wa kutokea mwishoni mwa msimu huu ambapo Juventus wanapiga hesabu za kuinasa saini yake. Kwenye Ligi Kuu England, Sanchez ameanzishwa mara nane tu katika mechi 17 msimu huu.

LONDON, ENGLAND.SUPASTAA wa Manchester United, Alexis Sanchez anaripotiwa kuweka mfukoni karibu Pauni 5 milioni kwa kukaa tu kwenye benchi msimu huu.

Fowadi huyo anayelipwa mshahara wa Pauni 505,000 kwa wiki amekuwa na maisha magumu huko Old Trafford tangu alipojiunga Januari mwaka jana akitokea Arsenal.

Maisha yake Sanchez kwa sasa huko Old Trafford yamekuwa yakukaa kwenye benchi tu.

Amefunga mabao matano tu katika mechi 41 alizoichezea timu hiyo kwenye michuano yote na huenda akafunguliwa mlango wa kutokea mwishoni mwa msimu huu ambapo Juventus wanapiga hesabu za kuinasa saini yake. Kwenye Ligi Kuu England, Sanchez ameanzishwa mara nane tu katika mechi 17 msimu huu.

Katika mechi hizo 17 alizocheza, amefunga bao moja tu na kuasisti mara tatu. Kwa mujibu wa takwimu za Bwin ni kwamba, Sanchez ametumikia dakika 917 kwenye benchi, ikiwa ni sawa na Pauni 5,323 kwa dakika na Pauni 4,881,014 kwa ujumla wake. Kutokana na hilo, Sanchez anashika namba moja kwa wachezaji wanaovuna pesa nyingi kwenye Ligi Kuu England kwa kukaa tu kwenye benchi.

Staa wa Liverpool, Daniel Sturridge anashika namba mbili kutokana na kuvuna Pauni 4,646,207 kutokana kutumikia dakika 2,353 kwenye benchi, ikiwa nyingi kuliko mchezaji mwingine yeyote yule kwenye ligi hiyo.

Mastaa wawili wa Manchester City, Riyad Mahrez na Nicolas Otamendi wapo kwenye nafasi ya tatu na nne kwa kuvuna Pauni 4,411,053 na 3,776,832 mtawalia.