Samatta na mastaa wengine Ulaya wanaocheza mwanzo mwisho

WIKI hii soka limenoga zaidi kwani Jumanne na Jumatano moja kati ya mashindano makubwa ya mchezo wa soka wa duniani Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA) imeanza kutimua vumbi.

Katika mashindano hayo imeshuhudiwa Mtanzania na nahodha wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta akiweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza ligi hiyo na rekodi nyingine ya kufunga bao, pamoja na timu yake ya Genk kupokea kipigo cha mabao 6-2 dhidi Redbull.

Samatta na wanasoka wengine Baada ya kutoka Ligi ya Mabingwa Ulaya kesho Jumamosi na keshokutwa Jumapili wanarudi Ligi Kuu za nchi wanazozitumikia.

Katika ushiriki wa mashindano mbalimbali wanasoka hukumbana na uchovu wa mwili ambao hutokana na misuli kufanya kazi sana wakati wa kucheza, hujulikana kama (muscle fatigue au physical fatigue) na huku nishati ikitumika.

Hali ya uchovu huweza kuwafanya wachezaji kupata hisia kama vile wanaumwa, hivyo hali hiyo isipoondoka mwilini huweza kumsababishia mchezaji kushindwa kucheza kwa kiwango.

Kwa wanasoka wengi wa kimataifa huweza kuidhibiti hali hiyo kupitia ushauri na maelekezo ya jopo la madaktari wa timu wakishirikiana na walimu wa viungo na wasingaji miili.

Haishangazi mchezaji kama Samatta aliyecheza usiku wa Jumanne kesho akicheza vizuri bila kuhisi uchovu, kutokana na huduma wanazofanyiwa.

Katika mazingira ya nchi zenye hali ya kitropiki ikiwamo Tanzania mchezaji mwenye uchovu uliotokana na kucheza mashindano mengi kwa kipindi kifupi anaweza kujihisi labda ana ugonjwa wa malaria. Mchezaji anaweza kucheza na uchovu lakini akacheza chini ya kiwango au akapata mkazo wa misuli na majeraha kirahisi.

Uchovu unatokeaje?

Misuli ya mwili ipo kama vile bunda lililoundwa na nyuzinyuzi zilizoshikamana zenye kuvutika na kutulia kama raba ngumu.

Wakati wa kufanya kazi misuli ya mwili hutumia nishati ya mwili ambayo ni sukari ili kuichoma na kupata nguvu ya kujongesha nyuzi za misuli ambazo zikivutika ndipo viungo vya mwili hufanya mijongeo kadhaa kama vile kukimbia, kuruka na kutembea.

Kujitokeza kwa uchovu unao ambatana na maumivu ni njia mojawapo ya mwili kujihami na kukupa ishara viungo vya mwili ikiwamo misuli imetumika kupita kiasi.

Wakati wa kufanya kazi na kutumia nishati hiyo ndipo huwapo na mrundikano wa zao ambalo hujulikana kitabibu kama tindikali ya lactic ambayo ndio sababu kubwa ya kuhisi uchovu mwilini kwa wachezaji. Tindikali hii ni zao la kuvunjwavunjwa kwa sukari iliyopo katika misuli na ni mojawapo ya taka mwili hivyo uwepo wake katika misuli ni sumu katika tishu, hivyo kuharibu afya ya misuli.

Uchovu unasababisha misuli ya mwili kukosa nguvu kama ilivyo kawaida yake na hii ndiyo sababu ya mchezaji mwenye hali hii kucheza chini ya kiwango na linaweza kuambatana na maumivu yanayoweza kuwa ya wastani mpaka kuwa makali. Hisia za uchovu huweza kuhisiwa zaidi katika maeneo ya maungio (joint), mgongoni, kiunoni, mapajani na magotini.

Vilevile uchovu unatokana na uwapo vitu vinavyoingilia hatua za ufanyaji kazi wa misuli yaani kukunjuka na kujikunja ili kuwezesha matendo mbalimbali ikiwamo kukimbia, kuruka na kutembea.

Tatizo hili linaweza kusababishwa pia na mishipa ya fahamu kutosisimua vizuri misuli na uwepo wa mrundikano wa mabaki au taka mwili baada ya seli kutumia sukari ya mwili kupita kiwango chake.

Uchovu unaweza kuchangiwa zaidi na mienendo na mitindo mibaya ya kimaisha ya mchezaji ikiwamo unywaji pombe au vilevi, matumizi ya tumbaku, kutopumzika na kulala saa za kutosha, kutokunywa maji mengi, msongo wa mawazo, mlo duni hasa ule usiokuwa na protini na kutokunywa maji mengi au kuwa na upungufu wa maji.

Jinsi ya kuukabili uchovu

Uchovu kwa mchezaji ni tatizo la muda linaloweza kuisha bila kupewa dawa lakini yapo mambo mbalimbali yanayondoa au kuzuia kupata uchovu kwa haraka na kwa urahisi. Mchezaji hutakiwa kunywa maji mengi ya kutosha lita 1-2 mara tu baada ya kumaliza mchezo. Vilevile anaweza kutumia matunda yenye majimaji ambayo humrudishua maji na sukari mwilini.

Ni kawaida pia kupewa vinywaji maalumu vya wanamichezo yaani ‘sports drinks’ ambavyo huwa na mchanganyiko wa maji, madini au chumvichumvi , protini, wanga na ladha.

Hupewa virutubisho vya ziada vya protini kabla na baada ya mechi kwani protini ndiyo inayokarabati mwili na kuwezesha misuli kufanya kazi kwa ufanisi.

Lishe hii inasaidia kukurudishia nguvu iliyotumika, kurudishia akiba ya nishati katika misuli na kuwezesha ukarabati na uponaji wa vijeraha vya misuli.

Wachezaji hupewa mazoezi ya viungo mepesi yanayonyoosha na kulainisha misuli angalau kwa dakika 5-10, mazoezi hayo hujulikana kama recovery exercise.

Mazoezi haya huleta uponaji wa misuli na husaidia kuondoa uchovu kwa haraka.

Mchezaji hupewa mapumziko katika eneo lenye hewa safi angalau kwa dakika 30-60, tofauti na kulala ambapo fahamu huwa haipo kupumzika unakuwa umetulia ukiwa macho pasipo kufanya kazi yoyote.

Anaweza kuingia katika huduma za usingaji yaani ‘body massage’ kisha baadaye akaingia katika mabafu maalumu ya kuoga au akaenda moja moja kuoga katika mabafu bila kusingwa.

Usingaji ni moja ya nyenzo kuu katika kukabiliana na uchovu na ndiyo maana ma staa kama Cristiano Ronaldo na Lionel Messi huwalipa maelfu ya dola wasingaji wao kutokana na huduma hiyo.

Kuoga katika mabafu maalumu huduma yenye kutoa mvuke ambao husaidia kuondoa takataka kirahisi mwilini kwani mishipa ya damu hutanuka, hivyo damu nyingi safi hufika katika misuli na kuondoa taka sumu.

Kupata mlo wa jioni ambao huwa si mzito sana uliosheheni wanga kiasi, mbogamboga na matunda na huku ukisheheni zaidi protini kama vile jamii ya kunde na samaki. Hutakiwa kupata mlo wa jioni saa mbili kabla ya kulala kwani kula na kulala kabla ya masaa hayo kunaongeza hali ya uchovu na mchoko.

Hutakiwa kulala saa 8 mfululizo katika eneo tulivu lisilo na usumbufu kwani kuukatisha katisha usingizi huweza kuunyima nafasi mwili kupumzika, hivyo kuuzidishia uchovu.

Kama uchovu hautaisha hata baada ya kupita saa 48 mchezaji anaweza kufanyiwa vipimo vya uchunguzi ila kubaini kama anaugua magonjwa mengine.

Haya ndiyo mambo ambayo wanasoka wa kulipwa wanayafanya ili kukabiliana na uchovu, hivyo kuwafanya kucheza tena bila uchovu.