Samatta awapagawisha Waturuki, asema mengine yanakuja

MABAO mawili aliyofunga nahodha wa timu ya taifa la Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta kwenye mchezo wake wa pili wa Ligi Kuu Uturuki ‘Super Ligi’ dhidi ya Fatih Karagumruk yamewapagawisha huko mashabiki wa Fenerbahce SK.

Samatta ambaye amejiunga na Fenerbahce SK siku chache zilizopita akitokea Aston Villa ya Ligi Kuu England, amewapa raha mashabiki wa timu hiyo baada ya kuisaidia kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Nahodha huyo wa Taifa Stars ambaye alianza kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha timu hiyo, alifungua akaunti yake ya mabao nchini humo katika dakika ya 24 kwa kuunganisha na mguu wake wa kushoto mpirawa kona iliyopigwa na nyota wa zamani wa Inter Milan, Caner Erkin.

Samatta aliendea kuonekana kuwa na njaa ya mabao kwenye mchezo huo kwani dakika ya 67 kipindi cha pili, aliendelea kuifanya Fenerbahce SK kuongoza kwa wigo wa mabao mawili baada ya kuunganishwa kwa kichwa krosi iliyochongwa na mchezaji wa zamani wa Bayern Munich ya Ujeruman, Jose Sosa.

Dakika ya 78, Fatih Karagumruk walipata bao kwa mkwaju wa penalti lililofungwa na Erik Sabo ambaye hata hivyo alipoteza nafasi nyingine ya mkwaju wa penalti dakika ya 87 wakati huo, Samatta alikuwa amepumzishwa huku nafasi yake akiingia Msenegal, Papiss Demba Cisse.

Cisse naye ni usajili mpya wa Fenerbahce SK, straika huyo ndiye aliyekuwa akitengeneza pacha ya hatari kwenye kikosi cha Newcastle United katika Ligi Kuu England alipotoka Samatta, miaka ya nyuma akiwa na Msenegal mwenzake Demba Ba.

Akizungumzia kiwango cha Samatta, Tolgahan Soylu ambaye ni shabiki wa Fenerbahce kupitia ukurasa rasmi wa mtandao wa kijamii wa Twitter wa klabu hiyo, alisema Samatta ndiye mfalme wao mpya.

“Hii ni tunu ambayo Aston Villa wametupa, nina hakika kama angeanza kwenye ile mechi iliyopita dhidi ya Gala tungewafunga wale. Binafsi natamani kumwona akicheza pamoja na Cisse kule mbele,” alisema.

Upande wa Instagram ya klabu hiyo ambayo walitupia picha ya Samatta akipachika bao lao la kwanza kwa guu lake la kushoto, Furkan Ertekin alisema natamani kusingekuwa na mapumziko ya wiki ya kimataifa hakika Samatta amejua kutupa furaha.

“Natamani Ligi ingeendelea tu, magoli ya namna ile ni muda kidogo sijaona. Hongera timu yangu kwa kazi kubwa na nzuri ambayo mmeifanya tumeweka pointi tatu kwenye begi,” alisema.

MSIKIE SAMATTA

Mfungaji huyo wa mabao mawili ya Fenerbahce mara baada ya mchezo huo akiongea na vyombo vya habari vya Uturuki, alisema, “Nadhani ni mchezo mzuri sana. Mambo yalikuwa magumu kidogo kwetu mwishoni. Lakini tunafurahi kuwa tumepata alama tatu. Hii ndio muhimu zaidi kwetu. Sasa tunahitaji kuangalia mbele. ”

Samatta aliongeza: “Nimefurahi sana kuisaidia timu yangu kwa kufunga mabao. Kama mshambuliaji, lengo langu bila shaka ni kufunga na ninaamini kuwa mabao mengine mengi yanakuja. Timu ni muhimu kila wakati kwangu.

“Ningependelea timu yangu kuwa bingwa kuliko kufunga hata mabao 100 halafu iwe kazi bure. Ninapofunga, ninafurahi kuisaidia timu yangu, lakini kama nilivyosema, jambo muhimu zaidi kwangu ni timu,” alisema.

Upande wake kocha wa Fenerbahce SK, Erol Bulut, alisema, “Mapumziko kati ya mechi ya kitaifa yatatufaa. Tutajaribu kurekebisha upungufu wetu kwa njia bora. Tunataka kutazama Fenerbahçe bora zaidi.”