Samatta atajwa mkutano mkuu TFF

Muktasari:

Ndumbaro amesema soka kwa sasa lina fursa nyingi za kiuchumi, utalii na kukuza lugha ya Kiswahili na kuwataka viongozi kuwa makini kuongoza sekta hiyo.

NAIBU Waziri wa Mambo ya Nje ya nchi, Damas Ndumbaro amemtaja Mbwana Samatta kuwa kielelezo cha utalii katika nchi nyingine kutokana na hatua aliyofika.

Samatta kwasasa anakipiga timu ya Genk ya Ubelgiji ambapo sasa anatajwa kusakwa na klabu nyingi Ulaya.

Ndumbaro amesema soka kwa sasa lina fursa nyingi za kiuchumi, utalii na kukuza lugha ya Kiswahili na kuwataka viongozi kuwa makini kuongoza sekta hiyo.

"Soka ni mchezo unaopendwa duniani kote hivyo lazima tuliangalie kwa jicho la tatu kufaidika nalo kwa mambo mbalimbali mfano nchi za Ulaya wachezaji wanajulikana kuliko viongozi,"

"Unaweza kukuta mtu anataja kikosi chote cha Manchester au Real Madrid na nyinginezo hiyo inaonyesha ni namna gani soka linapendwa,".

Amesema kwa hapa Tanzania ni Samatta ndiye amefanikiwa kufikia kiwango cha kuwa kama mastaa wa Ulaya na kwamba kuna haja ya kuwaandaa wengine watakaoungana naye.

"Kupitia wao Kiswahili kitazungumzwa na nchi nyingine, bendera ya Taifa itapepea wakitajwa kwamba ni Watanzania kwa sehemu watakayokuwepo kufanya kazi ya soka,"amesema.