Samatta arejea Ubelgiji na makali mapya

Monday January 14 2019

 

By Eliya Solomon

KRC GENK anayoichezea nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta imemaliza michezo yake miwili ya kujipima ubavu kipindi hiki ambacho Ligi Kuu Ubelgiji imesimama kwa wiki nne.

Samatta aliiongoza KRC Genk kucheza michezo miwili ya kirafiki kule Hispania ambako waliweka kambi kwa kucheza dhidi ya Fortuna Sittard ya Uholanzi na Schalke 04 ya Ujerumani.

Genk ilicheza mchezo wake wa kwanza Januari 10 dhidi ya Fortuna Sittard na kuifunga bao 1-0, lililopachikwa nyavuni na Samatta.

Katika mchezo wa pili, Genk ilitoshana nguvu, siku iliyofuata ya mabao 2-2 na Schalke 04.

Baada ya kumaliza michezo hiyo, Genk imerejea Ubelgiji ambako Ijumaa ya wiki hii, itaendelea na patashika za Ligi Kuu kwa kucheza dhidi ya Sint-Truiden.

Genk inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Ubelgiji ambayo ni maarufu kama Jupiler Pro, ikiwa imejikusanyia pointi 48 katika michezo 21 kwa kushinda 14, sare sita na imepoteza mara moja.

Advertisement