Samatta Afcon kwanza hiyo EPL isubiri

Muktasari:

  • Nje ya Bongo, ilipata nafasi ya kuongea na Samatta ambaye msimu uliopita aliingoza Genk kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Ubelgiji na kufuzu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, ambaye alisema lolote linaweza kutokea baada ya Afcon.

BAADA ya Mbwana Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji kuwa kwenye rada za Brighton, Aston Villa, Leicester City, Watford na Burnley, hatma ya mshambuliaji huyo, itafahamika zitakapomalizika fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2019 nchini Misri.

Samatta kwa sasa yupo Misri na kikosi cha timu ya Taifa (Taifa Stars) katika maandalizi ya wiki mbili kuelekea fainali hizo ambazo Tanzania inashiriki kwa mara ya pili tangu zianzishwe 1957.

Gazeti la The Sun la Uingereza liliripoti Juni 5 kuwa Brighton ndiyo wanaoongoza katika mbio za kuwania saini ya Samatta na tayari wameweka mezani Paun 12 milioni ambazo ni zaidi ya Sh. 35 bilioni.

Kwa mujibu wa The Sun, kocha wa zamani wa Brighton, Chris Hughton ni shabiki wa Samatta ambaye msimu uliopita alifunga mabao 23 kwenye Ligi Kuu ya Ubelgiji huku tisa akifunga kwenye Europa Ligi.

Mbali na kocha Hughton kumkubali sana Samatta, kiwango cha straika huyo wa zamani wa Simba na TP Mazembe, pia kimemvutia kocha wa sasa wa Brighton, Graham Potter.

Nje ya Bongo, ilipata nafasi ya kuongea na Samatta ambaye msimu uliopita aliingoza Genk kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Ubelgiji na kufuzu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, ambaye alisema lolote linaweza kutokea baada ya Afcon.

“Kuhitajika na klabu za England ni taarifa njema ambazo kwa sasa si vyema kuzizungumzia kutokana na majukumu yaliyopo mbele yangu, ila nimekuwa nikisema siku zote kuwa ni ndoto yangu ni kucheza Ligi Kuu England.

“Muda utaongea zaidi, nadhani lolote linaweza kutokea baada ya Afcon, siwezi kusema wapi naenda kwa sababu zote hizo ni tetesi,” alisema Samatta.

Wadau na mashabiki wa KRC Genk nchini Ubelgiji wanaamini kuwa huenda Samatta akaondoka dirisha dogo la usajili mwakani kutokana na tiketi waliyonayo ya kushiriki msimu ujao Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Jeff Megan ambaye ni Mtanzania anayeishi Ubelgiji, alisema vyombo vingi vya habari vimekuwa vikiripoti Imani ya wengi nchini humo kwamba si rahisi kwa Samatta kupoteza nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.

“Labda Samatta akajiunge na timu kubwa pale England zitakazompa hiyo nafasi, ukiziangalia Brighton, Aston Villa, Leicester, Watford na Burnley siyo timu ambazo zinashiriki Ligi ya Mabingwa,” alisema Megan.

Hata hivyo, Samatta aliiambia Mwanaspoti katika mahojiano maalum yaliyofanyika nyumbani kwake Ubelgiji mwezi uliopita kwamba kwake kucheza England ni jambo kubwa kuliko kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya na kwamba analenga kuwafungulia Watanzania milango ya kucheza katika ligi hiyo inayoongoza kwa kupendwa duniani.

Upande mwingine ambako sakata la Samatta linatazamwa kuhusu kutua kwake England ni mahusiano yake mazuri na nyota wa kimataifa wa Nigeria, Wilfred Ndidi ambaye alicheza naye KRC Genk kabla ya kujiunga na Leicester.

Pengine Samatta anaweza kwenda kuungana na swahiba wake huyo kwenye uwanja wa King Power unaotumiwa na vijana hao wa kocha wa zamani wa Liverpool, Brendan Rodgers kugonga glasi na kina Jamie Vardy.