Samatta, Ulimwengu watakata Stars

Wednesday October 07 2020
SAMATTA ULIMWENGU PIC

WACHEZAJI wanaocheza soka la kulipwa nje ya Tanzania, Mbwana Samatta (Fenerbahçe) na Thomas Ulimwengu (Tp Mazembe) wameonyesha utofauti kati yao na washambuliaji wanaocheza soka la kulipwa ndani ya Tanzania.

 

Katika mazoezi yanayofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, kocha Etienne Ndayiragije aliwapanga wachezaji wake kwa mafungu mafungu na ndipo wachezaji hao walionyesha umahiri katika kufunga.

 

Etienne aliwaweka Samatta na Ulimwengu katika makundi tofauti, na alikuwa anawataka wawe na umakini katika kufunga.

 

Advertisement

Zoezi hilo aliwachanganya na wachezaji wengine lakini nyota hao walikuwa wakifunga pindi wanapokuwa karibu na goli.

 

Pia Ndayiragije aliwataka wachezaji wake kuwa makini katika kukaba, hilo sio kwa beki tu bali hadi mshambuliaji na yeye alitakiwa kufanya hivyo.

 

Samatta alikuwa bora katika kupiga mipira kwa kukevu ambayo ilikuwa inaenda moja kwa moja wavuni.

 

Huku kwa upande wa Ulimwengu yeye alikuwa anatumia njia ya mashuti kufunga na hali hiyo ilikuwa changamoto hasa kwa makipa, Metacha Mnata na David Kissu ambao walikuwa wanafungwa na muda mwingine wanaokoa michomo hiyo.

 

Wakati huo huo mshambuliaji, Ditram Nchimbi na yeye alionyesha umuhimu wa nguvu zake katika kupambana na mabeki pamoja na kufunga.

 

Mazoezi ya Stars yalianza 10:25 na kumalizika saa 12:00 jioni.

 

Imeandikwa na Thomas Ng'itu, Olipa Assa, Eliya Solomon na Mustapha Mtupa.

Advertisement