Sakata la Kakolanya sasa liwalo na liwe

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwanaspoti, Richard alisema wamesubiri kwa muda sasa na walitakiwa wawe wamepata majibu tangu wiki iliyopita, japo wamewasilisha barua nyingine ili kuwakumbusha wahusika ndani ya muda waliokubaliana kuwa ifikapo Februari 6 wawe wamejibiwa lakini jana Jumatano walipowakumbusha waliambiwa leo Alhamisi ndio watapata majibu.

LILE sakata la kipa wa Yanga, Beno Kakolanya limeingia patamu baada ya Mwanasheria wa kipa huyo, Leonard Richard kusema kama Yanga watashindwa kutekeleza makubaliano yao, basi watachukua hatua wanazoona zinafaa kwa manufaa ya mteja wake.

Mwanasheria huyo alisema iwapo barua yao ya kuomba kuvunjwa kwa mkataba itachelewa kujibiwa basi itawabidi kuchukua hatua nyingine.

Akizungumza na Mwanaspoti, Richard alisema wamesubiri kwa muda sasa na walitakiwa wawe wamepata majibu tangu wiki iliyopita, japo wamewasilisha barua nyingine ili kuwakumbusha wahusika ndani ya muda waliokubaliana kuwa ifikapo Februari 6 wawe wamejibiwa lakini jana Jumatano walipowakumbusha waliambiwa leo Alhamisi ndio watapata majibu.

Aliongeza kutokana na tatizo hilo kushindwa kutatuliwa kwa wakati, wanatarajia kupeleka mgogoro wao huo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili waweze kuwasaidia kwani mteja wake hadi sasa yupo nyumbani hana cha kufanya huku mpira ikiwa ndio ajira yake.

“Maisha ya Kakolanya yanaendeshwa na kipaji chake na sasa ni muda mrefu hajafanya shughuli zake kutokana na mgogoro uliopo na kitu hicho kimejadiliwa kwa muda mrefu bila jibu muafaka, hivyo tunapenda kuwaarifu hatua nyingine itafuata baada ya kukaa meza moja kushindwa kutatuliwa,” alisema.

“Kwa upande wetu wepesi kutekeleza mambo tunayoambiwa na Yanga lakini wao hawafanyi hivyo, kwani tumekuwa tukiwaomba mara kwa mara kujibu ombi letu la kuvunja mkataba lakini wamekuwa wagumu kutujibu,” alisema.

Alisema sakata hilo lilikuwa chini ya Kaimu Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Omary Kaya lakini cha kushangaza jana amefanya mawasiliano naye na akapelekwa kaimu Mwenyekiti wa klabu hiyo Samwel Lukumay ili waweze kumalizana.