Sababu za Stars kufanya vibaya AFCON

Friday July 12 2019

 

BADO tupo kwenye kipindi cha kujitafakari baada ya timu yetu ya taifa 'Taifa Stars' kufanya vibaya kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zinazoendelea huko Misri.
Yalikuwa ni mashindano ambayo tuliingia kwa lengo la kujifunza hivyo ni wazi tumebaini masuala kadhaa ambayo kama tukiyafanyia kazi, soka la nchi yetu litainuka na tutafanya vizuri siku za usoni.
Kwa tathmini niliyoifanya kwa ushiriki wa Stars kwenye AFCON, nimebaini masuala kadhaa ambayo wadau wa mpira wa miguu tunapaswa kuunganisha nguvu zetu kuyashughulikia ili hapo baadaye tupige hatua.
1. UTEUZI  WA WACHEZAJI
Haukuzingatia uhalisia kwa kuwa wachezaji waliofanya vizuri kwenye ligi ya ndani hawakujumuishwa, mfano Jonas Mkude kwenye kiungo wa kukaba, Ibrahim Ajibu kupiga pasi za mwisho aliongoza Tanzania nzima eneo hilo na Salim Ayee kufunga na wengineo.
2. BODI YA LIGI
Kutokuwepo kwa bodi ya ligi inayoaminika kumechangia sana kubadilisha ratiba ya ligi mara kwa mara kwa misingi ya utashi au kutokuwa na weledi.
Hali hiyo imesababisha kuwepo kwa msimamo wa ligi usiokuwa na uhalisia na pia kuwafanya wachezaji kutokuwa na utimamu wa mwili endelevu.
3.LIGI KUKOSA WADHAMINI
Hii imesababisha kutokuwepo mazingira sawa miongoni mwa washindani ambao ni klabu, matokeo yake msimamo wa ligi hauakisi hali halisi ya ubora wa timu
4.WAAMUZI WA LIGI KUU
Kumeonekana wazi baadhi ya waamuzi kuzibeba baadhi ya timu na kuziangamiza baadhi ya timu huku Bodi ya Ligi ikifumba macho na masikio  ya wadau wake wakuu wanapolalamika na  kujikita zaidi kwenye kupangua ratiba bila ulazima na bila kuangalia athari za kiuchumi na kisaikolojia kwa timu.
5.WAANDISHI WA HABARI
Waandishi walitumia kalamu zao kuipamba Taifa Stars kwa sifa ambazo hawana  au tuseme hawajafikia.
6.UONGOZI WA TIMU YA TAIFA
Uongozi huu uwe na mchanganyiko ambao unabeba taswira ya Taifa badala ya uliopo sasa ambao unaonesha taswira ya wasanii na viongozi wachache tena waliopo Dar es Salaam
7.SULUHISHO
Kwa maoni yangu ni vyema TFF ikaweka nguvu kubwa kwa vijana U23, U20, U17, na kurejeshwa kwa mashindano ya mikoa ambako kutaleta hamasa kubwa na kupata wachezaji wenye vipaji kwa njia rahisi mno n.k huku serikali nayo ikiimarisha mashindano ya  shule za msingi na sekondari.
Imeandikwa na Dk. Athumani Kihamia ambaye ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambaye pia ni mdau na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga.

Advertisement