Sababu TPLB kutembelea klabu hizi hapa

Muktasari:

Kasongo alisema msimu ujao kanuni ya leseni za klabu zinaanza kutekelezwa hivyo ili kuziokoa klabu imebidi wakutane nazo ili kuhakikisha zinajiweka tayari.

Dar es Salaam. Bodi ya Ligi (TPLB) imeeleza sababu ya ziara inazofanya kuzitembelea klabu mbalimbali, huku ikijielekeza kuangalia changamoto zinazozikabili ili msimu ujao zishughulikiwe.

Mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi, Almas Kasongo alisema jana kuwa walianza ziara yao wiki iliyopita katika mikoa ya Nyanda za juu Kusini inayojumuisha Iringa, Njombe, Mbeya, Ruvuma, Lindi na Mtwara ambako walizitembelea klabu za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza.

Kasongo alisema msimu ujao kanuni ya leseni za klabu zinaanza kutekelezwa hivyo ili kuziokoa klabu imebidi wakutane nazo ili kuhakikisha zinajiweka tayari.

“Kama unavyojua Bodi ya Ligi ni chombo cha klabu, iko kwa ajili ya kutatua changamoto za klabu na kama viongozi tuko hapa kufanya kazi kwa niaba yao. Ndio maana tukaona tuanze kuzitembelea klabu ili kuwasikiliza changamoto wanazokutana nazo ili sisi kama watendaji waliotupa dhamana tuone jinsi gani ya kuzitatua na wao wabaki salama,” alisema.

“Kamati ya TFF ya leseni za klabu ni kamati huru ambayo haiiingiliwi, na kamati hiyo imesema msimu ujao wanaaanza kutekeleza kanuni ya leseni za klabu.

“Tukaona tusikae kimya, turudi kwa klabu tuwaambie kuwa kanuni hiyo itaanza kutumika msimu ujao, hivyo kama hawapo vizuri ni wakati wa kurekebisha ili waweze kupata leseni ya kushiriki ligi, lakini kama wako vizuri waboreshe zaidi.”

Kasongo alisema katika ziara hiyo wamewaambia viongozi wa klabu wanatakiwa kufanya vitu kwa kuangalia uwezo wao na siyo kulazimisha vile ambavyo hawana uwezo navyo na mwisho kuwaaachia madeni kutoka kwa wachezaji na benchi la ufundi.

“Mfano mmoja wa kanuni ya leseni ya klabu ni kuhakikisha haidaiwi na mchezaji yeyote, kocha au mtu yeyote wa benchi la ufundi, pia kuwa na mwanasheria, ofisa habari mwenye vigezo vya kuwa katika nafasi hiyo na vingine vingi ambavyo klabu inatakiwa kuhakikisha inatimiza ili iweze kupata leseni ya kushiriki ligi msimu ujao,” alisema.

Kasongo alisema hivi sasa wanaandika ripoti na kufanya majumuisho ya ziara waliyofanya kabla ya kuanza ziara nyingine kuelekea katika klabu zilizo Kanda ya Ziwa. Kanda hiyo inajumuisha mikoa ya Shinyanga, Mara, Kagera, Geita na Simiyu.

Maoni ya klabu

Katibu wa Prisons, Ajabu Kifukwe alisema uamuzi wa Bodi ya Ligi kuzitembela klabu ni mzuri.

“Zamani viongozi walikuwa wanatutumia kanuni tunazisoma na kurudisha mrejesho, lakini hawa wameona waje kwanza ili kujua changamoto zetu na kukumbushana mambo muhimu ambayo klabu inatakiwa kufanya,” alisema.

“Hili suala la leseni za klabu ni kitu ambacho kipo dunia nzima ila Tanzania ni kama tunaoneana haya na kuacha tu busara zitumike. Mfano katika leseni za klabu imesemwa lazima iwe na uwanja, siyo lazima uwanja wako kabisa lakini hata kama umekodi lazima mkataba uonyeshe kuwa katika mechi zote kusiwe na tukio lolote litakalozuia mechi kufanyika.”

Kifukwe alisema: “Pia klabu isiwe inadaiwa na wachezaji wala makocha yaani tuajiri watu kulingana na uwezo wetu ili tumudu kuwalipa. Pia kitu tulichozungumza na uongozi wa Bodi ni kila timu kabla ya ligi kuanza ipeleke bajeti ambayo asilimia 60 ionyeshe jinsi tutakavyoendesha timu bila kutegemea mdhamini.”

“(Hatua hii ni) ili hata kama tukiambiwa leo hakuna mdhamini timu ziweze kushiriki ligi kwa kumudu gharama zote ikiwemo usafiri wa kuwatoa sehemu moja kwenda nyingine na pia timu ijiendeshe kupitia vyanzo vyake vya ndani vya mapato.”

Naye Katibu wa Namungo FC yenye maskani mjini Ruangwa mkoani Lindi, Ally Selemani alisema suala la leseni ya klabu ni matakwa ya kikanuni, hivyo ni wajibu wa kila timu kulitekeleza ingawa anaamini klabu nyingi hazitatekeleza kwa asilimia 100.

“Ni jambo zuri viongozi wa Bodi ya Ligi walilofanya kuzitembelea klabu na kukumbushana mambo mbalimbali. Ila hili jambo la leseni za klabu linatakiwa kutekelezwa lakini kwa jinsi timu nyingi za hapa nchini zilivyo ni ngumu kutekelezeka kwa asilimia 100,” alisema Selemani.

“Klabu nyingi ni maskini kwani moja ya kanuni inasema kila klabu lazima iwe na timu ya wanawake, timu za vijana za rika tofauti, sasa bila pesa utaweza vipi kutekeleza hilo? Ni ngumu lakini tutajitahidi.”

Msemaji wa Ihefu FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, Peter Andrew alisema ujio wa Bodi ya Ligi katika klabu yao umewasaidia kwa kuwa kuna baadhi ya vitu wameweza kuvijua vizuri zaidi tofauti na mwanzo.

“Walifika hapa tukaongea vitu vingi na walituelekeza jinsi timu inavyotakiwa kuendeshwa, masuala ya uongozi na vitu gani kama klabu tunatakiwa kuvifanya ili kutekeleza suala la leseni ya klabu,” alisema Andrew.

“Kwa kiasi kikubwa kama sisi baadhi ya vitu ambavyo vinatakiwa katika leseni ya klabu tunavyo ikiwemo uwanja, basi na timu za vijana.”