SAMATTA: Mlima mgumu Aston Villa

JANUARI 21, 2020 mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta alitimiza ndoto yake kucheza Ligi Kuu England, baada ya kusajiliwa na Aston Villa ya inayoshiriki ligi hiyo.

Samatta ‘Poppa’ alikamilisha dili hilo akitokea KRC Genk ambako tangu kuwasili kwake 2017 akitokea TP Mazembe ya DRC Congo, alifanikiwa kutupia mabao 47 katika mechi 101.

Samatta alifika Villa na kuanza kuusoma mchezo, kabla ya kocha wake Dean Smith kuanza kutumia kwenye mchezo wa kwanza wa Kombe la Carabao Cup, dhidi ya Leicester City ambao hata hivyo alitolewa kipindi cha pili, huku timu yake ikishinda mabao 2-1.

Hata hivyo, Samatta amesajiliwa na timu hiyo yenye maskani yake Villa Park na kuikuta ikiwa kwenye janga la kushuka daraja, licha ya kikosi chao kutumia zaidi ya paundi 144.5M za usajili, lakini bado timu hiyo haipati matokeo ya kuridhisha kwenye Ligi Kuu.

Kwa sasa Aston Villa inashika nafasi ya 19 ikiwa na pointi 25, ni hatari zaidi itakayofanya timu hiyo ishuke daraja endapo mikakati thabiti haitafanyika, pengine ni ipi nafasi ya Villa kulingana na nafasi yao.

BADO WANA NAFASI YA KUBAKI ?

Aston Villa imecheza michezo 28, kwa maana imebaki michezo 11 kabla ya Ligi kumalizika, timu inayoshika nafasi ya 15, Brighton mpaka inayoshika nafasi 18, Bournemouth wote wa pointi 27, wamepishana na Villa pointi mbili, kwa kuzingatia kuwa Villa ina mchezo mkononi.

Kwa tafsiri ya haraka endapo Villa atashinda mchezo mmoja, atapanda nafasi ya 15 ambayo inashikiliwa na Brighton, hivyo wote watakuwa wana michezo sawa 29, Villa itahitaji pointi 15 kufika nafasi ya tisa inayoshikiliwa na Arsenal, walau kuwa na uhakika wa kubaki na kuwaombea wenye nafasi kuanzia 16 wapoteze.

MLIMA MGUMU WA KUPANDA

Katika michezo iliyobaki michezo sita, ni dhidi ya Arsenal, Liverpool, Man United, Chelsea, Everton na Wolverhampton, kiuhalisia hizo sio timu za kubeza, hivyo inahitajika mikakati na mipango kazi ili walau kuambulia chochote.

Kibaya zaidi miongoni mwa hizo timu, zote zipo katika nafasi ya kusaka nafasi ya Ligi ya Mabingwa na Ligi ya Europa, hivyo kwa namna yoyote na ubora walionao watataka kuhakikisha wanashinda michezo yao ili kupata nafasi hizo.

TATIZO LA ASTON VILLA NI HAPA

Aston Villa ni timu ya pili iliyofanya matumizi mengi ya pesa, kwenye usajili msimu huu, baada ya Man United, ila matokeo chanya ya usajili wao hayaonekani. Villa ina shida kwenye eneo la ulinzi limekuwa likuruhusu mabao hovyo, hali ambayo kama haitafanyiwa kazi safari itawahusu.

Villa imeruhusu mabao 56, ndiyo timu ya kwanza iliyoruhusu mabao mengi katika ligi nne kubwa duniani ikiwemo Bundesliga, La Liga, Seria A na EPL, ikiwemo na Lecce ya Italia yenye idadi hiyo ya mabao. Walau eneo la ushambuliaji linajitahidi kusaka mabao wamefunga 36, ila tatizo huwa hayachelewi kurudi.

NINI KIFANYIKE KUJINASUA

Kwanza Villa wanatakiwa kuhakikisha wanashinda mchezo wao wa kiporo dhidi ya Sheffield United, licha ya ugumu wa mchezo huo, na baada ya kushinda watakuwa wameongeza pointi tatu za uhakika.

Kocha Smith anatakiwa kuhakikisha safu ya ulinzi inatengenezwa vizuri ili kupunguza kuruhusu mabao hovyo, na pengine kurejea kwa Wesley kunaweza kusaidia eneo la mwisho sambamba na Mbwana Samatta.

NAFASI YA SAMATTA

Wakati Samatta anasajiliwa kwenda Aston Villa, baadhi ya vilabu vikiwemo Bournemouth, Everton na Brighton vilionesha nia ya kumhitaji, licha ya kuwa wenyewe Brighton wapo katika mstari mwekundu wa hatari ya kushuka.

Kwa maana hiyo huenda, klabu kama Bournemouth na Everton vikatupa ndoano kwa Samatta endapo timu yake itashuka daraja, licha ya kuwa kwa upande mwingine ni ngumu ila ni huenda timu hizo zikawa bado zinavutiwa na huduma yake.

KUREJEA TENA KWA DEAN SMITH

Bila shaka katika kipindi hiki cha virusi vya corona, ambao ligi hiyo ilisimama, ni wazi kuwa kocha Smith atakuwa ameangalia na kuumiza kichwa ni namna gani anaweza kuokoa jahazi lake kuepuka kuzama kwenda Championship.

Kama ligi hiyo itarejea Juni, Aston Villa ataanza nyumbani Villa Park kupambana na Chelsea ya Frank Lampard ambayo inaonekana kuwa vizuri ikitengenezwa na wachezaji vijana kwa sasa.