Ruvuma Queens waifanyia umafia Alliance Girls

Muktasari:

Ruvuma Queens wamepata jumla pointi nne kwa Alliance Girls msimu huu kwani katika mchezo wa kwanza ambao ulichezwa katika uwanja wa Maji Maji Songea timu hizo zilitoka suluhu (0-0).

UNAIKUMBUKA ile mechi iliyopita ambayo Alliance Girls waliitandika Panama Queens mabao 11-1 katika uwanja wa Nyamagana? sasa unaambiwa leo mambo yameenda ndivyo sivyo kwani nao wamechapwa 4-1 na Ruvuma Queens katika dimba hilohilo.

Alliance ambao waliingia uwanjani wakiwakosa beki wao hatari wawili Enekia Kasonga na Ester Mabanza ambao wanatumikia adhabu ya kadi nyekundu, walianza kuchapwa bao la kwanza na Amina Ramadhani dakika ya 19.

Dakika mbili baadaye Alliance walipachika bao la kusawazisha kupitia Janeth Matulanga, lakini kabla kipindi cha kwanza hakijaisha, Amina Ramadhani alirejea tena kambani kwa kutandika mkwaju mkali ndani ya 18 dakika ya 42.

Hata hivyo Ruvuma hawakulizika kwani waliendelea kushambulia lango la Alliance Girls na kupata bao la tatu kupitia kiungo mshambuliaji wao Aidati Zembindezi dakika ya 53 kabla ya Diana Lucas kufunga kitabu cha mabao dakika ya 90.

Akizungumza na Mwanaspoti Kocha wa Ruvuma Queens Mohammed Mwamba alisema walijua wanacheza na timu nzuri ndio maana walifanya maandalizi ya kutosha hivyo matokeo hayo walitegemea kuyapata.

"Tumefurahi kupata ushindi, Alliance ni timu kubwa kuliko yetu, ipo Ligi Kuu kwa zaidi ya misimu mitatu sisi ndio mara ya kwanza, tulifanya maandalizi ya kutosha maana tulijua tukizembea tu lazima tufungwe" alisema Mwamba.

Aliongeza baada ya ushindi huo ambao umewafanya wafikishe alama 34 sasa umeongeza nguvu ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake msimu huu kwani waliteteleka walipochapwa na Simba Queens katika mechi ya kwanza ya mzunguko wa pili.