Ruto arudia tena ahadi ya viwanja

Muktasari:

Miaka sita iliyopita wakati wa kampeni za uchaguzi, Ruto na mdosi wake Rais Uhuru Kenyatta waliahidi kuwa serikali yao ingejenga viwanja vitano vya kisasa katika Miji ya Eldoret, Mombasa, Garissa na Nakuru.

NAIBU Rais, William Ruto amewageuzia tena mashabiki wa kispoti hapa nchini kwa kutoa ahadi nyingine nzito kuhusu ujenzi wa viwanja vya kisasa.

Sasa badala za zile tano zilizoahidiwa mwaka 2013, Ruto ameahidi 11.

Miaka sita iliyopita wakati wa kampeni za uchaguzi, Ruto na mdosi wake Rais Uhuru Kenyatta waliahidi kuwa serikali yao ingejenga viwanja vitano vya kisasa katika Miji ya Eldoret, Mombasa, Garissa na Nakuru.

Hata hivyo, mpaka wa leo hamna uwanja hata moja waliofanikiwa kuusimamisha huku mhula wao ukiwa umesalia na miaka mitatu na miezo mitano kuisha.

Akifafanua ni kwa nini serikali ilifeli kujenga viwanja hivyo vitano ndani ya miaka minne kama ilivyoahidi, Ruto alisema:

“Mpango wetu wa ujenzi wa viwanja hivi bado upo palepale. Tulitenga muda ila kwa bahati mbaya tukashindwa kwa sababu tulirudia uchaguzi na kutumia zaidi ya Sh13 bilioni ambayo sehemu yake ilikuwa imetengewa ujenzi wa viwanja hivi.

“Lakini sasa tumejipanga upya na tumekusanya hela za kutosha kuendelea na mikakati hii,” Ruto alisema.

Na licha ya kuwa ni dhahiri muda unawapa kisogo kabla ya mhula wao wa pili kumalizika, Ruto ametoa ahadi mpya ya ujenzi wa viwanja 11 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

“Unaweza ukathibitishiwa na Wizara ya Michezo, tutajenga viwanja 11 kufikia mwisho wa mwaka huu au mwisho wa robo ya mwaka ujao. Hilo nahakikisha viwanja 11, inawezekana na itatendeka licha ya muda mdogo tulionao,” Ruto alisisitiza.

Kauli yake inaonekana kukinzana na ile ya Katibu wa Kudumu wa Michezo, Kirimi Kaberia ambaye Februari mwaka huu alisema serikali haina uwezo wa kujenga viwanja vitano vya kisasa ila itajitahidi kuhakikisha inasimamisha angalau kimoja kufikia 2022 kabla ya Rais Uhuru kung’atuka.