Ronaldo nitaacha soka nikifikisha miaka 40

Muktasari:

Ronaldo alifunga mabao matatu kwenye mchezo mmoja 'hat trick' yake ya kwanza akiwa na Manchester United kwenye mchezo ambao waliitandika Newcastle United, Januari 12, 2008 mabao 6-0.

Mshambuliaji wa Juventus na timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo ameweka wazi hana mpango wa kutundika daruga mwishoni mwa msimu huu wa 2019/20.

Mreno huyo mwenye umri wa miaka 34, alisema bado na uwezo wa kuendelea kucheza soka kwa kiwango kikubwa cha ushindani hadi akifikia miaka 40.

"Sina mawazo ya kuachana na mpira. Pengine naweza kuwa na mawazo hayo nikifikisha miaka 40 au 41, ninauwezo wa kuendelea kucheza. Zawadi ya kipaji nilichonacho natakiwa kuendelea kukifurahia," alisema.

Ronaldo alimaliza msimu uliopita wa Ligi Kuu Italia ‘Serie A’ akiwa kinara wa mabao wa Juventus kwa kufunga magoli 21, yaliyoisaidia klabu yake kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.

Mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United na Real Madrid amechukua ubingwa wa Ligi za ndani kwenye mataifa matatu tofauti England, Hispania na Italia.

Aliongeza; "Kuna wanasoka mwenye rekodi zaidi yangu, sidhani kama wapo ambao wanaweza kunizidi."

Ronaldo, ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa dunia wa mwaka mara tano sawa na nyota wa FC Barcelona, Lionel Messi ambaye kwa sasa anasumbuliwa na majeraha.