Ronaldo aizamisha Barca kwa bao la hewani, gumzo

Muktasari:

TOLEO lililopita Mwandishi Luca Caioli aliichambua mechi ya La Liga kati ya Barca na Real Madrid iliyopigwa Oktoba 7, 2012 na kumalizika kwa sare ya 2-2 huku Messi na Ronaldo wakionyesha ubora wao, baada ya hapo Caioli alianza kuichambua mechi ya Kombe la Mfalme baina ya timu hizo iliyopigwa mjini Valencia. Endelea…

TOLEO lililopita Mwandishi Luca Caioli aliichambua mechi ya La Liga kati ya Barca na Real Madrid iliyopigwa Oktoba 7, 2012 na kumalizika kwa sare ya 2-2 huku Messi na Ronaldo wakionyesha ubora wao, baada ya hapo Caioli alianza kuichambua mechi ya Kombe la Mfalme baina ya timu hizo iliyopigwa mjini Valencia. Endelea…

‘Out of this world’ lilisomeka gazeti la michezo la Marca na kufafanua kwa kuelezea jinsi Messi na Ronaldo mabao yao mawili waliyofunga na kuonyesha viwango kwa sababu wao ni bora duniani.

Na pia kuna matukio mengi ya kukumbukwa, Ronaldo kwa mfano hatasahau bao alilofunga Aprili 20, 2011 katika mechi ya fainali ya Kombe la Mfalme mjini Valencia, ni bao pendwa la mwaka la mashabiki ambalo lilitosha kuipa Real taji lake pekee la msimu.

Hata hivyo, taji hilo halikupatikana hadi katika dakika ya 100, Ronaldo alianza katika eneo la namba 9, eneo ambalo katika hali ya kawaida hafurahii kucheza, baada ya vita kali ya dakika 90 na soka la kuvutia, Ronaldo alikuwa na shuti moja tu lililolenga lango.

Alilazimika kusubiri hadi dakika za nyongeza ili kumaliza ukame wake wa mabao dhidi ya Barca, Di Maria alichezeshana na Marcelo, na Marcelo akapiga krosi kutokea upande wa kushoto na mpira kumzidi Alves, na hapo Ronaldo akaonyesha umahiri wake wa kupaa hewani aliojifunza wakati akiwa Man United na kuujaza mpira wavuni kwa kichwa.

Kipa wa Barca, Pinto hakuwa na la kufanya kuuzuia mpira huo, bao hilo lililotosha kuipa Real Madrid taji la kwanza la Kombe la Mfalme ikiwa ni takriban baada ya miaka 10.

Vipi kuhusu Messi katika mechi hii? “Ni kama vile alivurugwa, alijaribu kusukuma mambo yaende kutoka eneo lolote alilokuwa katika ushambuliaji lakini hakuwa na bahati,’’ lilisema Gazeti la El Pais katika uchambuzi wake wa mechi hiyo. “Yale makali yake ya ‘zigizaga’ yalikumbana na kikwazo kutoka kwa wachezaji wa Real Madrid, alijaribu kuutawala mchezo kwa mbali, kipindi cha kwanza timu yake ilipata tabu hata kupeana pasi za maana.

“Baada ya mapumziko kila kitu kilibadilika na pasi za ndani zilikuwa za maana bahati mbaya bao pekee ambalo angelifunga lilipuliziwa filimbi ya kuotea, mwishowe akabaki na nafasi yake ya kiuongozi akijaribu kuongoza mchezo jambo ambalo liliwapa nafasi Real Madrid kuwasumbua.”

Huo ulikuwa uchambuzi uliokwenda vizuri na pia ilikuwa mara ya kwanza kwa Barca ya Pep Guardiola kufungwa katika hatua ya fainali.

Na hapo hapo tusisahau mechi iliyofuata kwenye dimba la Nou Camp mwaka uliofuata ambako Ronaldo alibadili matokeo na kuwa sare ya bao 1-1 katika dakika ya 73 na hivyo kuiwezesha Real Madrid kutwaa taji la La Liga katika msimu wa 2011/12.

Pia, unapoamua kumzungumzia Messi ni vigumu kusahau kuzungumzia kiwango chake katika mechi ya Aprili 27, 2011 kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu, hiyo ilikuwa mechi ya kwanza ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Ni mechi ambayo iliipeleka moja kwa moja Barca kwenye hatua ya fainali ambayo mechi yake ilipigwa England kwenye Uwanja wa Wembley na Barca kubeba taji lao la nne la Ligi ya Mabingwa.

Ni mashambulizi mawili ya kasi na yenye maana ambayo yalizaa mabao mawili ya ushindi yote yakifungwa na Messi ambaye aliifanya Real Madrid kuja na mbinu ya kumiliki mpira huku wakilinda zaidi eneo lao. Tangu kuanza kwa mchezo, Real Madrid ilichokuwa ikikifanya ni kujaribu kumzuia Messi asicheze kwa staili yake iliyozoeleka, lakini hapo hapo hawakuwa wakifanya juhudi zozote kucheza au kuja na staili yao ya uchezaji.

Ilikuwa hivyo hivyo kiasi kwamba baada ya kama robo saa hivi, Ronaldo alionekana kuchoka na kuwataka wachezaji wenzake watoke katika maeneo yao ili aweze kucheza nao, na ili waweze kumtengenezea nafasi za kucheza.

Mwishoni mwa kipindi cha kwanza ni Ronaldo huyo huyo aliyetengeneza nafasi nzuri ya kupata bao kwa Real Madrid baada ya kumuweka Valdes katika wakati mgumu juhudi ambazo baadaye ziliungwa mkono na shuti alilopiga Ozil.

Hadi hapo juhudi za Ronaldo zilionekana katika tukio hilo tu na ndilo linaloweza kuzungumziwa lakini kwa upande wa Messi yeye alicheza kati zaidi, aliwekwa mbali na eneo la ‘boksi’ ambako angeweza kusababisha madhara.

Itaendelea Jumanne.