Robben huyo anukia Leicester City

Friday May 24 2019

 

London, England. Klabu ya Leicester City imedaiwa kujiandaa kumrejesha England, nyota mkongwe wa Bayern Munich, Arjen Robben.

Robben amewahi kutamba England akiwa na Chelsea kati ya mwaka 2004–2007 akiichezea mechi 67 na kufunga mabao 15 kabla ya kutimkia Real Madrid na baadaye kwenda kutua Munich aliyojiunga nayo tangu mwaka 2009 hadi sasa.

Inaelezwa kuwa The Foxes imevutiwa kumsajili nyota huyo wa kiuholanzi kwa vile hatakuwa na dau la usajili, kwani mkataba wake na Bavarian umeisha na mechi yake ya mwisho akiwa na uzi wa mabingwa hao wa Bundesliga itakuwa Fainali ya Kombe la Ligi wikiendi hii dhidi ya RB Leipzig.

Hata hivyo inadaiwa kuwa, Mholanzi huyo ana nia ya kurejea klabu yake ya zamani ya PSV Eindhoven ya nchini kwao.

Robben alinukuliwa akisema; "Sio kitu rahisi kufanya uamuzi. Kama unaamua kuendelea kucheza ni lazima utafute mahali ambapo patakuwa sahihi. Sio kwa ajili ya soka tu, lakini hata kwa familia yangu."

Advertisement