River Plate yaichapa Boca Juniors yatwaa Copa Libertadores

Monday December 10 2018

 

Madrid, Hispania. Hatimaye mzizi wa fitina ulikatwa jana kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu mjini Madrid, Hispania kwa River Plate kuwanyamazisha mahasimu wao wa mji wa Buenos Aires, Argentina, Boca Juniors baada ya kuifunga kwa mabao 3-1 katika mechi ya pili ya Fainali ya Kombe la ubingwa wa Amerika ya Kusini, maarufu kama Copa Libertadores.

Bocar Juniors ilitangulia kupata bao lakini ikaawaruhusu mahasimu wao River Plate kusawazisha na kufunga mabao mawili zaidi kuwawezesha kutwaa ubingwa wa Amerika ya Kusini, Copa Libertadores.

Timu hizo zililazimika kusafiri umbali wa zaidi ya maili 6,000, hadi Uwanja wa Santiago Bernabeu mjini Madrid, Hispania kucheza mechi ya pili ya Fainali ya Copa Libertadores baada ya ile ya awali kumalizika kwa kufungana mabao 2-2 nchini kwao Argentina.

Vurugu zilizofanywa na mashabiki wa Plate waliolipopowa kwa mawe basi la Boca Junior na kuwajeruhi baadhi ya wachezaji katika mechi ya pili ya Fainali hizo iliyokuwa ipigwe mwezi uliopita zilisababisha fainali hiyo kuahirishwa na baadaye kuhamishiwa nchini Hispania. 

Katika mechi hiyo ya jana ambayo mahasimu hao wa jiji la Buenos Aires, walicheza mbele ya mashabiki 72,000, Dario Benedetto ndiye aliyeanza kuifungia Boca Juniors bao la kuongoza dakika ya 45.

Hata hivyo, Lucas Pratto aliisawazishia Plate bao la kusawazisha mwanzoni mwa kipindi cha pili, matokeo yaliyodumu hadi dakika 90 zinamalizika na hivyo kulazimika kuongezwa dakika 30 ndipo River Plate wakazitumia vizuri kutwaa ubingwa.

Baada ya kuanza kwa dakika 30 za nyongeza Boca Junior walipata pigo la kwanza kutokana na Wilmar Barrios kulimwa kadi nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.

Plate wakalitumia pengo hilo vyema kwa kujipatia mabao mawili yaliyofungwa na Juan Quintero dakika ya 109 na Gonzalo Martinez akaongeza la tatu muda mchache baadaye kuipa ushindi wa 3-1, hivyo kutwaa ubingwa wa Copa Libertadores kwa jumla ya mabao 5-3.

Licha ya kuwa pungufu na kuwa nyuma kwa mabao 3-1 bado vijana wa Boca Junior walipambana vikali na nusura Gonzalo Martinez aipatie mabao dakika za lala salama hata hivyo mpira wake mmoja uligonga mwamba na mwingine ukapanguliwa na kipa.

Huo ulikuwa ubingwa wa nne kwa River Plate katika michuano hiyo tangu kuanzishwa kwa Copa Libertadores mwaka 1960.

Advertisement