Rio asema Bruno anambeba Pogba

Muktasari:

Viungo hao wawili wamekuwa wakifanya vyema pamoja kwenye kikosi hicho cha Man United tangu msimu uliporejea baada ya janga la corona na timu imeshinda mechi nne tangu wakati huo

LONDON, ENGLAND. RIO Ferdinand amesema Bruno Fernandes ametua mzigo mkubwa uliokuwa ukimkabili Paul Pogba na kumsaidia Mfaransa huyo kuanza kucheza soka tamu akifurahia maisha Manchester United.

Viungo hao wawili wamekuwa wakifanya vyema pamoja kwenye kikosi hicho cha Man United tangu msimu uliporejea baada ya janga la corona na timu imeshinda mechi nne tangu wakati huo.

Hofu ilikuwa kubwa kama wachezaji hao wangeweza kucheza pamoja, lakini jambo hilo halipo tena na viungo hao wawili wamekuwa habari nzito ndani ya uwanja.

Kiwango cha Pogba kimekuwa juu kwa sasa kwenye kikosi cha Man United baada ya huko nyuma kuwa majanga makubwa na Ferdinand anaamini hilo linatokana na uwepo wa Fernandes.

“Paul Pogba amekuwa mchezaji tofauti tangu ligi iliporejea,” alisema Ferdinand.

“Kiwango cha soka lake kwa sasa, kinadhihirisha ada ya Pauni 89 milioni kumnasa Pogba miaka minne iliyopita.

“Sababu kubwa ni moja tu ni mtu anayecheza naye kwenye kiungo, Bruno Fernandes. Pogba kwa sasa wala hana presha ya kutaka kuonyesha kitu chochote yupo. Solskjaer bila ya shaka anafurahia namna wawili hao wanavyocheza.”

Wachezaji hao wawili walipokuwapo wakati Man United ilicheza soka la kuvutia wakiwachapa Bournemouth 5-2 Jumamosi iliyopita, huku Fernandes akimaliza mchezo kwa kufunga na kuasisti mara mbili, wakati Pogba alihakikisha timu inakuwa salama kwenye sehemu ya kiungo kuhakikisha timu inashinda.

Tangu alipowasili United Januari, Fernandes ameonyesha kuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi hicho, akihusika kwenye mabao 11 katika mechi tisa alizocheza kwenye Ligi Kuu England.

Ferdinand alisema analofanya Fernandes limemwondolea presha na majukumu Pogba yeye ndiye anayepaswa kufanya vizuri ili timu ishinde.