Rich Mavoko arudi, atambulisha menejiment mpya

Friday August 7 2020

 

By Nasra Abdallah

MSANII Rich Mavoko amerudi rasmi kwenye sanaa baada ya kuwa kimya muda mrefu huku akitambulisha menejimenti mpya ambayo itakuwa ikimsimamia.

Menejimenti yake hiyo ambayo ameitaja kuwa ni Pilipili Entertainment ameitambulisha leo Ijumaa Agosti 7, 2020 katika mahojiano na kipindi cha 360.

Rich alisajiliwa na lebo ya WCB, Juni 2013 na ilipofika Agosti mwaka 2018, kuliubuka mvutano wa masuala ya mkataba kati yake na lebo hiyo hadi kufikishana Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kudai haki zake na mwisho wa siku kutangaza kuamua kufanya kazi kivyake.

Akiwa WCB aliachia nyimbo mbalimbali ikiwemo Ibaki Story wimbo wa kwanza kuufanya akiwa chini ya lebo hiyo, zikifuatiwa na nyingine kama Sheri alioimba na Fid Q, Show Me, Kokoro alioimba na Diamond, Rudi aliomba na msanii wa Nigeria Patoranking.

Wakati akiwa mwenyewe alichia nyimbo mbili ikiwemo Wezele, Usizunge na Ngegele na Babiloni

Katika mkataba huu mpya, Rich amesema kampuni yake ya Bilioneakid imeingia mkataba Pilipili Entertainment ambapo katika mapato yatakayopatikana kupitia kazi zake hizo za muziki watagawana nusu kwa nusu.

Advertisement

Akifafanua hili, amesema mbia mwenzake huyo atawekeza zaidi kwake katika mambo ambayo alikuwa hawezi kuyafanya ikiwemo uandaaji wa video zake.

Akieleza ujio wake, amesema leo Ijumaa anaachia albamu yake itakayokuwa na nyimbo nane na baada ya hapo atafanya ziara maeneo mbalimbali ili kuwafikia mashabiki wake.

Mkurugenzi wa kampuni ya Pilipili aliyetambulika kwa jina la Nilash, amesema katika ujio wa albamu wamewekeza zaidi ya Sh10 milioni kwa kuanzia.

Advertisement