Riadha Bara, Zanzibar washikana mashati

Thursday August 15 2019

 

By Yohana Challe

Dar es Salaam. Rais wa Chama cha Riadha Zanzibar (ZAA), Abdulhakim Chasama ametoa lawama kwa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) akidai limekuwa likifanya uamuzi bila kuwashirikisha.

Chasama alidai wamekuwa wakitoa malalamiko kwa viongozi wa RT, lakini hayafanyiwi kazi licha ya kutoa mchango kwa wanariadha.

"Tatizo hatushirikishwi katika uamuzi, mashindano yanayoshirikisha Muungano wa Tanzania yanatakiwa tukae vikao vya pande zote mbili, lakini hilo halifanyiki,”alidai Chasama.

Rais huyo alidai wameshangazwa na uamuzi wa RT kumteua Ali Gullam katika timu ya Taifa ya riadha inayoshiriki Michezo ya Afrika licha ya kupeleka idadi kubwa ya wanariadha wakitokea Zanzibar.

Tanzania itawakilishwa na wanariadha sita ambao ni Gabriel Geay, Benjamini Kulwa, Natalia Elisante, Regina Mpigachai, Sarah Ramadhani na Gullam.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa RT, Wilhelm Gidabuday alisema Zanzibar haishirikishwi kwa kuwa haijaruhusiwa kisheria kupiga kura ndani ya shirikisho.

Advertisement

Michezo ya Afrika ‘All African Games’ inafanyika kila baada ya miaka minne na mwaka huu itafanyika Rabat, Morocco Agosti 19 hadi 31, mwaka huu.

Advertisement