Rekodi ya Eto’o yawatesa mastaa AFCON

Muktasari:

  • Ili wafikie rekodi hiyo au kuivunja, mastaa wa sasa kama Mbwana Samatta, Sadio Mane, Mohammed Salah, Samuel Chukwueze wanapaswa kufunga idadi kubwa ya mabao kwenye fainali za mwaka huu kwani wengi wao hawajafikisha hata mabao matano kwenye fainali za AFCON.

LICHA ya baadhi ya mastaa kwenda kwenye fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka huu huko Misri wakiwa wametoka kutamba kwenye ligi mbalimbali duniani, nyota hao wana mlima mrefu wa kupanda ili kuvunja rekodi iliyowekwa na mshambuliaji wa zamani wa Cameroon, Samuel Eto’o kwenye fainali hizo.

Eto’o anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga idadi kubwa ya mabao kwenye mashindano hayo akiwa na kikosi cha Cameroon na hakuonekani dalili za mastaa wa sasa kuivunja kirahisi.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Real Madrid, Barcelona na Chelsea amefunga jumla ya mabao 18 katika awamu tofauti ya fainali hizo pindi alipoiwakilisha nchi yake akifuatiwa na nyota wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Pokou aliyefunga mabao 14.

Ili wafikie rekodi hiyo au kuivunja, mastaa wa sasa kama Mbwana Samatta, Sadio Mane, Mohammed Salah, Samuel Chukwueze wanapaswa kufunga idadi kubwa ya mabao kwenye fainali za mwaka huu kwani wengi wao hawajafikisha hata mabao matano kwenye fainali za AFCON.

Katika kizazi cha sasa, wachezaji pekee ambao angalau wamefunga mabao zaidi ya matano na pengine miujiza inaweza kutokea wakafikia au kuvunja rekodi ya Eto’o ni Andre Ayew wa Ghana mwenye mabao nane, Gervinho wa Ivory Coast (6) wakati Diuemerci Mbokani wa DR Congo, Salomon Kalou wa Ivory Coast na Wakaso Mubarak wa Ghana wana matano kila mmoja.