Real Madrid yawasubiri watoto watano wa Raiola

Wednesday March 25 2020

Real Madrid yawasubiri watoto watano wa Raiola,corona,Santiago Bernabeu,Mwanasport, virusi vya corona,

 

By Fadhili Athumani

CORONA inazidi kuleta changamoto mpya ya maisha ya binadamu. Ndio, dunia ina changamoto nyingi lakini kusambaa kwa virusi vya corona kumeleta balaa kubwa kwa sasa.

Moja ya njia za kudhibiti virusi hivi ni kuepuka msongamano kwa kujiweka mbali na ndio sababu michezo karibu yote imepigwa marufuku na mastaa wamejificha majumbani kwao.

Lakini kama kuna mtu ambaye agizo hilo la kujificha kwenye mijengo yake wala halijamtisha kabisa anajiita ‘Super-Agent’, Mino Raiola.

Kibonge mmoja hivi raia wa Italia mwenye pesa zake na mtu wa mipango muda wote. Huyu ni miongoni mwa mawakala wakubwa duniani na mwenye ushawishi mkubwa kwenye soka la Ulaya. Jamaa amezowea kufanyia kazi zake chini ya kivuli au ufukweni, tena akiwa amezungukwa na warembo kibao akila bata. Yaani anafanya kazi kwa bidii lakini kwa ustadi mkubwa.

Kifaa chake muhimu kabisa kwenye kazi zake ni simu na kazi yake nyingine kubwa ni kufuatilia yanayojiri michezoni. Muda wote macho na masikio yake huwa kwenye soka la usajili. Akishapata data anazotaka, kazi yake ni kupiga simu tu. Huyo ndio Mino Raiola.

Alhamisi iliyopita alinukuliwa akifichua kuwa amekuwa na uhusiano mzuri na Real Madrid katika kutekeleza majukumu yake. Pia, akafichua kuwa ana mpango wa kuwapelekea wababe hao wa Santiago Bernabeu mashine za kazi kwenye dirisha kubwa lijalo. Unafahamu ni mashine gani hizo? Mwanaspoti linakupatia zote.

Advertisement

PAUL POGBA (MAN UNITED)

Kama kuna taarifa ambayo imezungumzwa kwa muda mrefu basi ni kuhusu kiungo huyo kuachana na Manchester United. Dili lake lilisababisha kuibuka kurushiana maneno kati ya Mino na kocha wa Man United, Ole Gunnar Solskjaer.

Mino anataka kumuondoa mteja wake huyo na kumpeleka Real Madrid au Juventus, na mara kadhaa mpango wake huo umegonga mwamba kutokana na mabosi wa United kuweka dau kubwa ama kupuuza.

Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane ni shabiki mkubwa wa Pogba na ndiye amekuwa akiushinikiza uongozi wake kumsainisha ili atue Santiago Bernabeu.

Bado Man United imegoma kumuweka Pogba sokoni huku ikionya kwamba inaweza kusikiliza ofa kama kuna klabu itaweka mezani kuanzia Pauni 120 milioni. Lakini, taarifa mpya ni kuwa Rais wa Real Madrid, Florentino Perez yuko tayari kurudi mezani kusaka saini ya Pogba ambaye anapewa nafasi ya kwenda kuwa mrithi wa Luca Modric.

GIANLUIGI DONNARUMMA (AC MILAN)

Dili hili nalo limekuwa midomoni mwa wachambuzi wa soka kwa muda sasa. Tangu alipojipambanua kama kipa bora kwenye ulimwengu wa soka, Donnarumma amekuwa kipenzi cha mashabiki wengi wa Real Madrid.

Mwaka 2017, Raiola alithibitisha kuwa kwa uwezo wake kinda huyo

hastahili kuendelea kuitumikia klabu yake hiyo ya utotoni, kabla kabla ya kumsainisha mkataba wa Euro 6 milioni, na nyingine kwa ajili ya ndugu yake, Anthonio (Euro milioni moja).

Gigi Donnarumma yuko kwenye rada za Real Madrid kwa muda mrefu, lakini sasa ndoto ya kutua Santiago Bernabeu inaweza kutimia. Hata hivyo, Chelsea nayo inasaka huduma yake ili kwenda kuchukua nafasi ya Kepa Arrizabalaga.

Kwa sasa mashabiki wa AC Milan wana hasira dhidi ya kauli ya Raiola kwamba, Gigi alisaini mkataba mpya kwa presha ya kisaikolojia, aliposaini mkataba pamoja na mdogo wake. Mashabiki hao walijibu mapigo kwa kubeba mabango yakimtaka kipa huyo kuondoka klabuni hapo.

Inadaiwa kuwa kuanzia hapo Donnarumma hakuwahi kuonyesha furaha ya kuwepo San Sirro licha ya kiwango chake kuonekana kuwafurahisha mashabiki. Kwa kuwa amekuwa kwenye rada za Real Madrid kwa muda mrefu, Raiola anaamini wakati wa kuondoka San Sirro umefika.

MARCO VERRATTI (PSG)

Muitaliano mwingine ambaye yuko chini ya Raila. Kiwango chake kinazivutia Real Madrid na Manchester United ambayo hata hivyo haiwezi kumnasa kutokana na kuingia kwenye bifu la Raiola. Amekuwa kwenye mipango ya Zidane kwa muda mrefu. Kama kuna kiungo anayestahili kuitwa wa dunia basi ni Marco Verrati anayekipiga PSG ya Ufaransa.

Kumekuwa na tetesi nyingi kuhusu hatima ya Modric ndani ya Santiago Bernabeu na inaaminika kwamba, kama dili la Pogba litakwama basi Verrati atakwenda kuvaa jezi ya Madrid.

DONYELL MALEN (PSV)

Achana na habari za Frenkie de Jong, Mitthijs de Ligt na wenzake kule Uhalonzi, ishu kubwa ni kinda mwenye miaka 21. Huyu hapa mkali wa mabao wa PSV, Donyell Malen.

Mpaka sasa amefunga mabao 17 katika mechi 25 alizocheza. Wastani wake ni bao moja baada ya kila dakika 60. Melan alianzia soka lake pale Arsenal, lakini kwa sasa ni mmoja wa washambuliaji hatari duniani.Donyell anawindwa na vigogo Ulaya wakiwemo Barcelona na Arsenal wenyewe waliomkuza huku Real Madrid nao wakipewa nafasi kubwa.

HAALAND (BORUSSIA DORTMUND)

Wengi wanaweza wakaona bado ni mapema kuanza kujadili uwezo wake. Wengine wakiamini huenda akashika breki. Lakini, kwa anachokifanya kwa sasa huko Bundesliga hakuna ubishi huyu dogo atasumbua sana. Dunia iko tayari kwa maajabu ya Haaland, anayeichezea Borussia Dortmund kuja kuweka rekodi tamu kabisa kwenye soka.

Habari nzuri ni kwamba wakala wake ni Raiola, na habari mbaya zaidi kwa Borussia Dortmund ni kwamba Real Madrid wanafuatilia kila kitu kuhusu yeye.

Dortmund ni mabingwa wa kusaka vipaji, lakini wamekuwa dhaifu na kuanza kuzowea maisha ya kupokonywa mastaa wao wanaowapika klabuni hapo.

Wameamua kuwa wanyonge ili wavune pesa ndefu kwa kuuza wachezaji na hilo wamefanikiwa sana na muda ukifika basi hawatakuwa na uwezo wa kumzuia Haaland kwenda Madrid, Bayern Munich, Man United, Barcelona au PSG kama wakubwa hao watataka.

Katika mechi 11 akiwa na Borrusia, Haaland ametupia wavuni mabao 12 ikiwemo hat-trick yake ya kwanza kwenye mechi ya kwanza akiwa na wababe hao wa Signal Iduna Park.

Habari mbaya zaidi kwa Borrusia ni kuwa, mshambuliaji wa Kifaransa, Karim Benzema kilomita zimeanza kukata. Kwa sasa ana miaka 32, hivyo hana muda mrefu wa kuachana na wababe hao na kuondoka kwenye soka la ushindani.

Na hilo likitokea kwa haraka maana yake Zidane atamwambia Raiola kumleta dogo huyo kuungana na wenzake waliopo kikosini kwa sasa kama Rodrygo na Vinicius Jnr.

Advertisement