Real Madrid wamfanya Isco chambo cha kumnasa Paul Pogba

Thursday February 13 2020

Real Madrid wamfanya Isco chambo cha kumnasa Paul Pogba,REAL Madrid,Paul Pogba,Manchester United ,dirisha la usajili,

 

REAL Madrid imeripotiwa kufikiria kumtumia kiungo Isco kwenye dili la kumnasa Paul Pogba ili kuwalainisha Manchester United wafanye biashara hiyo wakati wa dirisha la usajili wa majira ya kiangazi litakapofunguliwa.

Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane bado anadaiwa kuhitaji huduma ya Mfaransa mwenzake, Pogba akimtaka kiungo huyo mshindi wa Kombe la Dunia aende akakipige Bernabeu. Los Blancos wanaamini kwa sasa itakuwa rahisi kumnasa Pogba baada ya Man United kufanikiwa kunasa saini ya kiungo wa Kireno, Bruno Fernandes.

Kwa mujibu wa El Desmarque Madrid imepanga kumjumuisha Isco kwenye ofa hiyo ya Pogba ili kupunguza bei yake, ambapo Man United inataka Pauni 150 milioni. Man United kwa siku za karibuni imekuwa ikihusishwa na Isco, huku Mhispaniola huyo akihitaji kuondoka baada ya kukumbana na wakati mgumu chini ya Zidane, ambapo alianzishwa mara tisa tu kwenye mechi za La Liga msimu huu.

Pogba amecheza mechi nane Man United msimu huu kutokana na kusumbuliwa na majeruhi.

Advertisement