Rayvanny, halaiki wanogesha ufunguzi Fainali za Afcon U17

Monday April 15 2019

 

By Thomas Ng'itu

MKALI kutoka WCB, Rayvanny ni baadhi ya walionegesha ufunguzi wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Vijana (Afcon) U17 uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Taifa, ambapo Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ndiye aliyekuwa mgeni rasmi.

Ufunguzi huo uliofanyika saa chache kabla ya timu ya taifa, Serengeti Boys kuvaana na Nigeria katika mchezo wao wa kwanza, ulianikizwa na halaiki ya wanafunzi wa Shule ya Gate Fountain ambao walifanya mautundu yao na kuwapa burudani mashabiki wachache waliojitokeza.

Nje ya uwanja kabla ya ufunguzi huo shamrashamra ya vikundi vya ushangiliaji viligonesha kabla ya Waziri kuzindua michuano hiyo akiwa sambamba na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Ahmed Ahmed aliyewasili mapema jana mchana.

Rayvanny aliyeingia uwanjani hapo kwa kusindikizwa na mabausa wake wanne alitumbuiza kwa nyimbo zake kali kabla ya kuwaachia kundi la Halaiki kufanya yao na kunogesha shoo hiyo ya uzuinduzi ambayo hata hivyo ilipooza kwa kuhudhuriwa na mashabiki wachache licha ya michuano hiyo kuwa mikubwa na kufanyika kwa mara ya kwanza nchini.

Kundi hilo la Halaiki lililoundwa na wanafunzi zaidi ya 50 lilikuwa kivutio kutokana na kuunda maumbo mbalimbali na kujipanga mistari ambayo aliyekuwa akiingalia alikuwa akiburudika kwa kutosha kutokana na kuvutia.

Walimu waliokuwa wanawasimamia walionekana kuwa makini muda wote kuhakikisha vijana wao hawakosei kile ambacho wanawaelekeza.

Utamu wa michuano hiyo kwa leo utahamia kwenye Uwanja wa Azam Complex ambapo mechi za Kundi B zitachezwa leo kwa Cameroon kuvaana na Guinea, huku Morocco kumenyana na Senegal.

Advertisement