Ratiba CAF yamvuruga Aussems

Muktasari:

Katika programu ya mazoezi anayofanya hapa tangu Simba ilipowasili, Aussems alikuwa akitilia mkazo zaidi mazoezi ya nguvu na mbinu za kupata ushindi.

Rosternburg. Ratiba ya michuano ya kimataifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), imeonekana kumchanganya Kocha wa Simba, Patrick Aussems.

Akizungumza jana, Aussems alisema ratiba ya CAF imevuruga programu yake ya mazoezi aliyopanga kuwapa wachezaji wa Simba nchini hapa.

Simba itacheza ugenini dhidi ya UD Songo la Msumbiji kati ya Agosti 9 na 11 kabla ya kurudiana Dar es Salaam kati ya Agosti 25 na 28, mwaka huu.

Aussems alisema hakutarajia Simba kuanza hatua ya awali katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo analazimika kupangua programu yake ili kwenda na muda mfupi uliobaki.

Alisema katika kuanzia sasa atabadili mfumo wa ufundishaji kwa kutoa mafunzo ya nguvu, ufundi na mbinu kwa pamoja kulinganisha na ratiba ya awali.

Katika programu ya mazoezi anayofanya hapa tangu Simba ilipowasili, Aussems alikuwa akitilia mkazo zaidi mazoezi ya nguvu na mbinu za kupata ushindi.

“Ndani ya siku mbili hizi wachezaji saba wa timu ya Taifa wataondoka na kurudi siku chache kabla ya mechi ,”alisema Aussems.

Wachezaji wa Simba walioko Taifa Stars ni kipa Aishi Manula, Jonas Mkude, Gadiel Michael, Ibrahim Ajibu, Erasto Nyoni, John Bocco na Mohammed Hussein.