Ratiba CAF: Gor Mahia, Sharks wanapata tabu sana

Monday November 5 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi, Kenya. Takribani saa 48 zimepita tangu Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), ikutane Jijini Rabat, Morocco kwa ajili ya kupata ratiba ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2018/19.

Baada ya kukutana kwa wajumbe hao wenye kauli kubwa kwenye masuala ya soka la bara hili, bado moshi mweusi umetanda angani, kwani mpaka sasa hawajatoa ratiba yenyewe kwa umma wa wapenda soka.

Hali hii inawatesa wawakilishi wa Kenya, katika michuano ya ligi ya mabingwa Afrika, Klabu ya Gor Mahia na wenzao Kariobangi Sharks, ambao wanashiriki kombe la shirikisho kwa mara ya kwanza. Mpaka sasa hawajui kinachoendelea na hawafahamu wapinzani wao. Wanapata tabu sana!

Kilichopelekea CAF kufikia uamuzi wa kufanya droo ya mechi za mtoano, inatokana na mabadiliko katika Kalenda ya michuano ambapo mechi za msimu mpya, zitaanza wakati kalenda ya msimu mwengine haujamalizika hivyo, ikabidi pafanyike namna ya kufanya mchujo.

Raundi ya kwanza ya mechi za mtoano, kwa msimu wa 2018-19, zimeratibiwa kuchezwa kati ya Novemba 27-28, ambayo ni takribani majuma mawili na nusu yajayo, ambayo itakuwa ni siku moja kabla ya raundi ya kwanza ya mechi za kombe la shirikisho (Novemba 30).

Wakati huo huo CAF, wamesema kama itatokea bingwa wa msimu huu akawa tofauti ambaye anaendelea na michuano hiyo, hakuna nchi hata moja ambayo itaruhusiwa kuwa wa wawakilishi wawili kwenye Kombe la Shirikisho.

Advertisement